• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Kindiki sasa abatilisha notisi zilizopandisha ada za pasipoti, vitambulisho kuruhusu maoni ya umma

Kindiki sasa abatilisha notisi zilizopandisha ada za pasipoti, vitambulisho kuruhusu maoni ya umma

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki amesitisha hatua ya wizara yake ya kupandisha ada zinazotozwa huduma mbalimbali zinatolewa na Idara ya Uhamiaji.

Hii ni baada ya Profesa Kindiki kufutilia mbali notisi aliyochapisha kwenye gazeti rasmi la serikali kuongeza ada hizo ikiwemo ile ya kupata kitambulisho cha kitaifa na ile ya pasipoti.

Kwa mfano kulingana na ilani hiyo, ada ya wanaotaka kupewa kitambulisho cha kitaifa, kwa mara ya kwanza ilipandishwa kutoka Sh100 hadi Sh1000, hatua ambayo ilipingwa vikali na Wakenya akiwemo kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Lakini akibadilisha hatua hiyo waziri Kindiki mnamo Jumanne alisema hivi: “Notisi inatolewa kwa umma kwamba Notisi Kwenye Gazeti Rasmi la Serikali Nambari 15239 ya 2023, 15240 ya 2023, 15241 ya 2023 na 15242 ya 2023 katika toleo rasmi la CXXVNO Nambari 239 iliyotolewa Novemba 7, 2023, na kuchapishwa na Waziri wa Usalama kuhusiana na kuongeza kwa ada na matozo mbalimbali kwa huduma zinazotolewa na Idara ya Uhamiaji na Huduma za Rais imefutiliwa mbali kutoa nafasi kwa ushirikishwaji wa maoni ya umma kuhusu suala hilo.”

Waziri huyo aliagiza Idara Uhamiaji kuendesha shughuli ya ukusanyaji maoni ya umma kuhusu suala hilo kufikia Desemba 10, 2023.

“Na idara hiyo imeagizwa kukamilisha shughuli hiyo haraka iwezekanavyo,” Profesa Kindiki akaongeza.

Waziri alisema mpango wa kubadilisha ada zinazotozwa huduma za Idara ya Uhamiaji unachochewa na haja ya kuifanya Kenya kujitegemea katika kufadhili Bajeti ya Kitaifa.

“Hatua hii inaondoa nchi katika minyororo na mzigo wa madeni ambao umegeuka tishio kwa uhuru wetu na heshima kwa vizazi vijavyo,” Profesa Kindiki akaeleza.

Kufikia sasa, watu wawili wamewasilisha kesi mahakamani kupinga kupandishwa kwa ada ya huduma za idara hiyo kama vile utoaji wa pasipoti miongoni mwa nyingine.

  • Tags

You can share this post!

Kivutio maarufu kwa watalii Kisumu ambacho kimegeuka Sodoma...

Kwa mara ya kwanza akina mama wa Kibajuni kisiwani Pate...

T L