• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Maonyesho ya ASK yasababisha upungufu wa maji Nairobi

Maonyesho ya ASK yasababisha upungufu wa maji Nairobi

NA SAMMY WAWERU

MAANDALIZI yanayoendelea ya Maonyesho ya Kimataifa ya Kibiashara na Kilimo Nairobi mwaka huu, yanayoandaliwa na Chama cha Kilimo cha Kenya – ASK yamesababisha upungufu mkubwa wa maji mitaa kadhaa Kaunti ya Nairobi.

Maonyesho hayo yatakayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Nairobi, yataanza Septemba 25, 2023 na yatafunguliwa rasmi na Rais William Ruto.

Imebainika kuwa usambazaji maji Nairobi, umeelekezwa Uwanja wa Jamhuri kwa minajili ya shughuli hiyo, jambo ambalo limechangia upungufu wa bidhaa hii.

“Tumeshuhudia upungufu wa maji kwa muda wa mwezi mmoja uliopita, na tunaelezwa kuwa hii ni kutokana na maandalizi yanayoendelea ya Maonyesho ya ASK,” akasema Joseph Mwangi, mmiliki wa jengo la kukodisha Zimmerman, Nairobi, katika mahojiano na Taifa Leo Dijitali.

Maeneo mengine yanayoathirika na upungufu wa maji ni pamoja na Githurai, Kasarani, Mwiki, Kahawa West, Kayole, Kariobangi, Mathare, Kibra, Lang’ata, na mengineyo.

Mitaa mingi Nairobi hupata ugavi wa maji kupitia Kampuni ya Usambazaji Maji ya Nairobi, ndiyo Nairobi Water and Sewerage Water.

Kampuni hiyo haijatoa taarifa yoyote kuhusu uhaba wa maji, hivyo kuwaacha wakazi kutafuta mbinu mbadala kwa gharama ya juu.

“Usambazaji wa maji ulisitishwa ghafla bila taarifa yoyote mapema,” akalalamika Bw James Mwangi, mmiliki wa ploti katika mtaa wa Githurai.

Sasa wakazi wanalazimika kutegemea wauzaji na wachuuzi maji, haswa wale wanaosambaza kwa kutumia mikokoteni, ambapo mtungi wa lita 20 unagharimu hadi Sh70.

“Kando na mfumuko wa gharama ya juu ya maisha, tunazidi kulemewa kununua bidhaa hii ambayo tayari tunalipia kupitia kodi ya nyumba,” alisema Daisy Kinyua, mkazi wa Zimmerman.

Maonyesho ya ASK Nairobi ni hafla ya siku saba itakayofanyika hadi Oktoba 1.

Maji yanayoelekezwa katika Uwanja wa Maonyesho ya Jamhuri, yanatumika kukuza mimea na mazao yatakayokuwa onyeshoni.

Kulingana na waandalizi, hafla hiyo imevutia zaidi ya waonyeshaji 350, kutoka ndani na nje ya nchi, ambao wamethibitisha kuhudhuria.

  • Tags

You can share this post!

Bilionea aliyeanzisha Equity Bank apigwa mnada

Wasioamini Mungu wataka kila familia iwe na mtoto mmoja

T L