• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Bilionea aliyeanzisha Equity Bank apigwa mnada

Bilionea aliyeanzisha Equity Bank apigwa mnada

NA SIMON CIURI

MALI ya mwanzilishi wa Benki ya Equity, bilionea Peter Munga itauzwa katika mnada kwa kushindwa kulipa mkopo.

Mali hiyo ya Bw Munga iko kaunti za Murang’a na Meru.

Arifa iliyotangaza kuuzwa kwa milki zake mbili, kampuni ya madalali ya Legacy Auctioneering Services, ilichapishwa katika vyombo vya habari mnamo Jumanne.

Mdokezi wetu alisema deni hilo ni la mamilioni ya pesa japo hakutaja kiasi kamili.

Bw Munga, anayemiliki mali nyingi zikiwemo shule ya kifahari, alikataa kujibu mawasiliano yetu naye kuhusu suala hili.

Arifa hiyo ilisema mali hizo zilitumika kudhamini mikopo iliyochukuliwa katika mashirika ya kifedha.

“Mali hizo ni ploti mbili zenye thamani kubwa mjini Murang’a zenye usajili Murang’a Municipality Block 11/234… Ukubwa wake ni hekta o.o830 ama ekari 0.205 hali ardhi nyingine yenye usajili nambari 235, ina ukubwa wa hekta 0.0644 ama ekari 0.159. Ploti hizi hazijastawishwa,” Legacy Auctioneering ilisema katika arifa.

Mbali na Bw Munga, pia rafiki yake wa kibiashara, James Gichanga Karanja ataathiriwa kama mmiliki mshirika wa mali zitakazouzwa.

Kutangazwa kuuzwa kwa mali za bwanyenye huyo zitafufua msururu wa kesi za zamani na za sasa ambapo mfanyabiashara huyo maarufu ameshtakiwa kwa kutolipa madeni.

Ardhi hizi, Legacy ilisema, zimeandikishwa kwa jina la Equatorial Nut Processors Ltd.

Katika mkopo uliochukuliwa arifa hiyo ya Legacy imetambua wadhamini kuwa James Gichanga Karanja na Peter Kahara Munga ambao ni wamiliki wa kampuni ya Equatorial Nuts Processors Limited.

Kiwanda cha kampuni ya Equatorial Nuts Processors kimejengwa kilomita chache kutoka mjini Maragua.

Kilianzishwa mwaka 1994 ili kutengeneza na kupakia nafaka za makadamia, njugu karanga na korosho.

Kiwanda hicho kimewaajiri wafanyakazi 1,000. Kampuni hiyo ya Equatorial Nuts huuza bidhaa zake nchini Amerika, Uingereza na Mashariki ya Mbali.

“Katika kipindi cha mwaka mmoja kiwanda hicho huuza bidhaa za zaidi ya Sh1 bilioni,” Bw Munga aliambia chombo kimoja cha habari wakati wa mahojiano mnamo 2015.

Wakati huo huo, madalali hao Legacy Auctioneering, walisema watauza kiwanda cha pamba cha Meru Ginnery Limited, kilichoanza kutoa huduma zake mnamo 1994.

Pia kiwanda hiki kilianzishwa na Bw Munga 1994.

Alieleza Taifa Leo mnamo 2015 kwamba alikinunua mwaka wa 2013 akiwa na lengo la kutengeneza taulo na sodo. Alieleza kwamba alikinunua kiwanda hicho baada ya “kunusa pesa” katika sekta hiyo ya pamba.

“Nisingejiingiza katika sekta hii ya pamba kama sikuwa na matarajio ya kupata faida. Viwanda vya kutengeneza nguo vina umuhimu mkubwa kwa kuwa nchi hii haifikii kiwango cha ubora ilichowekewa barani Afrika na shirika la AGOA,” Munga alisema wakati huo.

Kiwanda hicho cha Meru Ginnery Ltd kimejengwa katika ardhi ya ukubwa wa hekta 6.5 ambayo pia imestawishwa.

Ndani yake kumejengwa kiwanda cha kusaga pamba ya kutengeneza nguo, mashine za kupima, mabohari na vifaa vinginevyo.

  • Tags

You can share this post!

Sakaja atabasamu madiwani wa UDA wakiunga mkono...

Maonyesho ya ASK yasababisha upungufu wa maji Nairobi

T L