• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Maonyesho ya kilimo Nakuru kupamba moto

Maonyesho ya kilimo Nakuru kupamba moto

NA MERCY KOSKEI

KAMPUNI na mashirika 150 yanatarajiwa kuhudhuria Maonyesho ya Kitaifa ya Kilimo (ASK) 2023 mjini Nakuru.

Maonyesho hayo yatakayofanyika Julai 12 hadi Julai 17, ni ya pili tangu makali ya janga la Corona yapungue na kuisha ambalo lilisababisha makala ya hiyo kusitishwa kwa miaka miwili.

Mwenyekiti wa ASK tawi la Nakuru Perminus Migwi alisema kuwa wako tayari kwa maonyesho ya kilimo ya kila mwaka ambayo yamevutia washirika wengi.

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari, Bw Mwigwi alifichua kuwa waonyeshaji 80 tayari wamejiandikisha na wengine zaidi wanatarajiwa kuwasili wiki hii.

Kati ya waonyeshaji waliosajiliwa, 11 ni wapya, wakiwa ni Benki ya Access, Dayosisi ya Nakuru na Muungano wa Wakulima wa Kenya miongoni mwa wengine.

Hii, kulingana na Bw Migwi, ni ishara kuu ya kuchipuka vyema kwa maonyesho ambayo yaliathirika vibaya na janga la Covid-19.

Mojawapo ya eneo la ASK Nakuru, maandalizi yako kipindi cha lala salama. Picha|MERCY KOSKEI

“Mwaka huu tunatarajia onyesho kurejea kwa ukubwa wake kamili baada ya janga la Corona. Ningependa kuwakaribisha wageni, wanafunzi na waonyeshaji  kwa wingi, na ninawaahidi maonyesho mazuri ya kujifunza na kuburudika,” Bw Migwi alisema.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘kukuza kilimo cha kuzingatia hali ya hewa na mpango wa biashara kwa ukuaji endelevu wa uchumi’, ambayo Bw Migwi alisesema kuwa inawiana na uhalisia wa athari hasi za mabadiliko ya hali ya hewa (climate change).

Mifumo ya malipo ya kidijitali imeanzishwa ili kuruhusu wageni kulipia kiingilio mapema.

Ada ya kuingia inasalia kuwa ile ile, huku watu wazima wakilipa Sh250, watoto Sh200 na wanafunzi wa shule za upili Sh150.

Maonyesho ya ASK Nakuru ni mojawapo ya matukio kongwe zaidi ya kilimo katika eneo hilo, yanayoangazia Kaunti za Bonde la Ufa la Kati Nakuru, Narok, Kericho, Nyandarua na Laikipia.

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Mwanamuziki John Njagi anavyolima mahasidi wake kwa cheche...

Ungekuwa jaji, ungewafanyia nini waliomng’oa macho...

T L