• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Mwanamuziki John Njagi anavyolima mahasidi wake kwa cheche za matusi kiusanii     

Mwanamuziki John Njagi anavyolima mahasidi wake kwa cheche za matusi kiusanii     

NA MWANGI MUIRURI

MWANAMUZIKI wa ngoma za ushauri John Njagi anafahamika kwa ueledi wa kusuta wanaomkera kwa maneno mazito ambayo hugonga kama kombora.

Nyimbo zake kama Múgwí wa Útukú (mshale wa usiku) na Múndú útoí úngí (asiyemfamu mwingine), ni kati ya ngoma mbili zake ambazo huwa ni matusi kwa mahasidi wake.

Katika wimbo huo wa Mùgwî, Njagi huimba kwamba “watu wa kwenu walitupasha kukuhusu kuwa hata umezalisha mbuzi”, wewe ukidhania ni ya ukunga shari yako.

Katika huo wimbo mwingine, Njagi huskika akitoa onyo kwamba “wewe endelea…lakini iwapo nitakupata ukiongea kunihusu ndio utajua cha ngariba sikuwa nimekiendea mtoni kuteka maji ya utengenezaji matope”.

Anaendelea kumtolea hasidi huyo vitisho kwamba “mimi sio tu usanii ambao umenipa umaarufu bali najua mengine mengi”.

Anamuwazia mabaya kiasi kwamba anamfananisha na mchawi ama mwizi katika jamii ya Agikuyu ambaye “adhabu yako ingekuwa kuvuliwa nguo kisha ukunjwe utoshee mzinga wa nyuki ukiwa umefungwa kwa majani makavu, upigwe kiberiti kisha uachwe ubingirike hadi kwa mto uage dunia”.

Anaongeza kuwa msanii huyo alikuwa amemkera sana kupitia usambazaji udaku na hata licha ya kutumana mara kadha ili akanywe, alikosa kuambilika wala kusemezeka.

“Ndio, nyimbo hizo zilimlenga mmoja wa wasanii wenzangu ambaye alikuwa amenikera sana kiasi kwamba nilionelea tu adhabu muafaka zaidi ilikuwa nimsute kwa maneno makali ili apate adabu,” asema Njagi.

Njagi anasema kwamba “hizo ngoma mbili hazikuwa moto licha ya wengi kusema zilikuwa za kugonga ndipo kama makombora ya kuelekezwa kwa kompyuta.

“Nilikuwa nimejiandaa kisawasawa kutoa fataki baada ya fataki…Kama vile shujaa wa kivita wa Kimaasai hurusha mkuki akiwa amehifadhi mwingine kwa kumkanyaga kwa guu lake…Ni bahati alipata kuwa nyimbo hizo mbili zilimfanya akunje mkia na akakoma udaku,” akasema.

Lakini kwa sasa Njagi ambaye katika usanii hufahamika kama “kanda ya Kanunga” anakubali kuwa alizidi mipaka ya ufaafu wa lugha na udhibiti wa hasira.

“Ni kama nilikosea na ninaomba msamaha na nawashauri wasanii wenzangu dhidi ya kuchukua mwelekeo huo wa kuanika upungufu wa akili kwa mashabiki wetu wapendwa”.

Njagi anasema kwamba “Nisameheeni…Nimetubu mara kadha, na ujumbe wangu ni kwamba tunapaswa sanasana kuimba ngoma za kuburudisha au kuelimisha mashabiki wetu wala sio za kutwangana na kudunishana”.

Wakati haimbi za matusi, Njagi huwa katika ngoma za kupigia debe mapenzi, heshima kwa wazazi na wazee, vipenzi wa kike na pia mahaba.

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Padri wa Kanisa la Katoliki apatikana ameaga dunia kwenye...

Maonyesho ya kilimo Nakuru kupamba moto

T L