• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Mjukuu wa mzee wa kijiji aliyetuhumiwa kuiba maharagwe Murang’a auawa na raia 

Mjukuu wa mzee wa kijiji aliyetuhumiwa kuiba maharagwe Murang’a auawa na raia 

Na MWANGI MUIRURI

MZEE wa kijiji Kaunti ya Murang’a anaomboleza kifo cha mjukuu wake, aliyefumaniwa akipakia maharagwe ya wizi katika msitu.

Tukio hilo la Jumatano jioni, liliishia mjukuu huyo aliyekuwa miongoni mwa wengine wanne kuandamwa, akanaswa na hatimaye kupigwa hadi kufariki.

“Ni ukweli kuwa mtoto huyo aliyetambuliwa kama Boniface Thuo na ambaye ni mjukuu wa mzee wa kijiji Bw Francis Kaigu aliuawa na raia katika Kijiji cha Kihingo kilichoko eneo bunge la Kigumo,” akasema Kamanda wa polisi Murang’a Bw Mathiu Kainga.

Kabla ya kuuawa, kijana huyo alishinikizwa kuwataja washirika wake katika wizi.

Umati huo ulitekeleza msako katika nyumba ya mshukiwa mwingine, ambapo nyama za mbuzi zinazosemekana kuibwa Kijiji cha Kirima zilipatikana na kutwaliwa.

“Ushahidi wa kuibwa kwa mbuzi wanne wa Bw Bonny Nyangi na kisha kuchinjwa na kupikiwa kwa nyumba hiyo ulipatikana. Bado tunasaka waliohepa,” akasema Bw Kainga.

Huku akiwashinikiza wenyeji kutochukua sheria mikononi mwao, na badala yake kukabidhi maafisa wa polisi washukiwa wa uhalifu ili waadhibiwe kisheria, afisa huyo aliwataka vijana wa eneo hilo wakome kushiriki wizi.

Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Bw Patrick Mukuria tayari amelalamikia kuongezeka kwa visa vya wizi wa mavuno na pia mifugo akiamrisha kamati za usalama kuwajibikia changamoto hiyo.

 

  • Tags

You can share this post!

Kindiki aahidi vitambulisho na pasipoti kutolewa ndani ya...

Wolves wahakikishia mashabiki Lopetegui ataendelea kuwa...

T L