• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Mlipuko wa meli watikisa Mombasa

Mlipuko wa meli watikisa Mombasa

KEVIN ODIT Na KARIM RAJAN

MTU mmoja alijeruhiwa katika mlipuko uliotokea ndani ya meli ya mafuta iliyokuwa imetia nanga karibu na kituo cha meli cha African Marine kilichoko Liwatoni, Likoni.

Akithibitisha kisa hicho, mkuu wa polisi wa kituo cha Central, Bw Maxwel Agoro, alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mlipuko huo ulisababishwa na mrundikano wa gesi ndani ya matangi ya kusafirisha mafuta kwenye meli hiyo.

Bw Agoro alisema meli hiyo kwa jina East Wind II ilisafirisha mafuta hadi Zanzibar kabla ya kurejea kutia nanga Mombasa.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa polisi, mtu aliyejeruhiwa alikimbizwa katika Hospitali ya Pandya.

“Ni gesi iliyojaa kwenye chumba cha mafuta na ilitaka kutoka. Ni kama unapokuwa na chombo kilicho na mafuta ndani yake, na baada ya kumwaga mafuta na kufunika chombo, hata ikiwa ni kitupu, kitavimba. Katika harakati za kutafuta njia ya kutokea, gesi haikupata njia na ndipo mlipuko ukatokea,” alisema Bw Agoro.

Mlipuko huo mkubwa ambao ulitetemesha majengo mjini hadi umbali wa kilomita mbili, ulisababisha moto ambao uliharibu sehemu za meli hiyo.

Hata hivyo, hatua za haraka za Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) iliyotumia maboti na magari ya zimamoto yaliyofika hapo haraka, zilizuia uharibifu zaidi.

Watu waliokuwa eneo la tukio waliondolewa haraka na vikosi vya dharura.

Vikosi vya pamoja vya wapelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai, Polisi wa Kupambana na Ugaidi, na Kitengo cha Kutegua Mabomu vilitembelea eneo la tukio ili kufahamu kilichojiri.

Walioshuhudia tukio hilo walisema mlipuko huo uliambatana na wingu la moto lililoruka na moshi mweusi.

Mlinzi katika moja ya majengo karibu na kituo hicho alisema vyuma pia vilirushwa angani kutoka kwenye meli huku wananchi wakikimbia kutafuta usalama.

  • Tags

You can share this post!

Mungai Eve, Trevor wanusurika kwenye ajali

Gachagua: Pombe imepungua, watoto wanazaliwa

T L