• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 4:55 PM
Sabina Chege: Raila angeshinda urais mwaka 2022 ikiwa angeniteua mgombea-mwenza wake

Sabina Chege: Raila angeshinda urais mwaka 2022 ikiwa angeniteua mgombea-mwenza wake

NA WANDERI KAMAU

MBUNGE Maalum Sabina Chege amesema kwamba kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, angeshinda urais mwaka 2022, ikiwa angemteua kuwa mgombea-mwenza wake.

Mnamo Jumatano, Bi Chege alisema anaamini ana ushawishi wa kutosha ambao ungemwezesha Bw Odinga kupata uungwaji mkono wa kutosha kutoka kwa wenyeji wa ukanda wa Mlima Kenya.

Bw Odinga alimteua Kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua, kuwa mgombea-mwenza wake kwenye uchaguzi huo, uliofanyika Agosti 9, 2022.

Bi Chege alikuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa wakimfanyia kampeni Bw Odinga katika ukanda huo na sehemu nyingine nchini, baada ya kuraiwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kutotetea nafasi yake ya Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Murang’a, aliyokuwa akiishikilia.

 “Sikuwania nafasi yoyote kwani nilitaka kuupigania mrengo wa Azimio la Umoja. Licha yetu kutukanwa, tulimfanyia kampeni ‘Baba” (Raila), katika kila sehemu nchini. Mliniona wenyewe kwenye kampeni hizo. Kwa wakati mmoja, nilitajwa kuwa miongoni mwa viongozi ambao wangeteuliwa kuwa mgombea-mwenza miongoni mwa wanasiasa wanawake. Ikiwa tu wangenipa nafasi hiyo, tungeibuka washindi,” akasema.

Bi Chege ni miongoni mwa viongozi wa Chama cha Jubilee (JP) waliohama kutoka Azimio na kujiunga na mrengo tawala wa Kenya Kwanza, unaoongozwa na Rais William Ruto.

Kwa sasa, Bi Chege anashikilia kuwa ndiye kiongozi rasmi wa chama hicho, baada ya ‘kumpindua’ Bw Kenyatta.

  • Tags

You can share this post!

Mombasa yameremeta Krismasi ikibisha hodi

Afueni kwa wasafiri baina ya Lamu na Garsen mawe yakipangwa...

T L