• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Polisi wawinda wahalifu waliovamia dukakuu la Shivling

Polisi wawinda wahalifu waliovamia dukakuu la Shivling

NA WYCLIFFE NYABERI

POLISI mjini Kisii wanachunguza jinsi watu wasiojulikana walivyoingia katika mojawapo ya matawi ya dukakuu la Shivling mnamo Jumatano usiku.

Idadi ya isiyojulikana ya wezi wa mabavu, waliingia kwenye duka hilo lililo karibu na St Jude’s Flats kwa nia ya kuiba pesa taslimu.

Hata hivyo, polisi wamekataa kudokeza mengi kuhusu swala hilo na kusema kulizungumzia kutahatarisha uchunguzi ambao tayari umeanza.

“Suala hilo ni nyeti na tunalichunguza kwa karibu. Tafadhali niruhusu nisilizungumzie kwa sasa,” Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kisii ya Kati, Bw Isaac Kimwele ameambia Taifa Leo kwa simu.

Watu wengi ambao walikuwa wamefika mjini Kisii asubuhi, walifurika kwenye duka hilo kujionea kitakachojiri baada ya habari hizo kuenea.

Maafisa wa polisi walipoarifiwa kuhusu tukio hilo, walilizingira jengo hilo lakini hakuna jambazi aliyepatikana kufikia Alhamisi adhuhuri.

Mmoja wa waendeshaji bodaboda, ambaye mara kwa mara huwa ameegesha pikipiki sehemu nje ya dukakuu hilo akisubiri wateja, alisikika akisema kuwa kamera za CCTV za duka hilo ziliharibiwa na majambazi hao zizinase picha zozote.

“Milango inayoelekea kwenye baadhi ya vyumba humo ndani imevunjwa. Inaonekana walikuwa wakitafuta pesa,” mwendeshaji huyo wa pikipiki alisikika akisema.

Mnamo Julai 2023, mtu mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa majambazi walipotekeleza uhalifu katika eneo la Suneka ambalo liko karibu umbali wa kilomita saba kutoka mji wa Kisii baada ya majambazi kuvamia dukakuu jingine.

Majambazi tisa waliokuwa na silaha, walivamia Moraa Supermarket saa nane usiku mkuu na kuanza kufyatua risasi hewani.

Baada ya kuingia ndani ya eneo hilo, majambazi hao waliokuwa na bunduki aina ya AK47 na bastola walisonga mbele ambapo wapigahesabu walikuwa wakihesabu fedha kutokana na mauzo ya siku hiyo na kuanza kuwamiminia risasi.

Walitoroka na kiasi cha pesa kisichojulikana kutumia pikipiki ambayo haikuwa na nambari za usajili.

Majambazi hao walimuua mlinzi wa dukakuu hilo.

Wafanyakazi wengine wawili, walipata majeraha ya kichwa kila mmoja na sehemu nyingine za miili.

Maganda ya risasi tatu zilizotumika yalipatikana katika eneo la tukio ambapo polisi na wapelelezi walichukua kwa uchambuzi.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi ‘born town’ wanavyokimbilia vijijini kula...

Mwigizaji Bwire Ndubi aomba msaada wa kifedha kupata...

T L