• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Jinsi ‘born town’ wanavyokimbilia vijijini kula githeri msimu wa Krismasi, Mwaka Mpya

Jinsi ‘born town’ wanavyokimbilia vijijini kula githeri msimu wa Krismasi, Mwaka Mpya

NA MWANGI MUIRURI

KATIKA miaka ya hadi Milenia ya 2000, githeri kilikuwa chakula cha kawaida katika familia nyingi za eneo la Kati na kuna baadhi ya watu hata walikuwa wakikihusisha na umaskini.

Waliozaliwa na kuzoea maisha ya mjini lakini wenye mizizi katika eneo hilo, mara nyingi walikiona kuwa ni chakula kisicho na thamani hata kidogo.

Ulichohitajika kufanya katika eneo hilo ni kuingia kwa ghala na kuchota mahindi na maharagwe yaliyokuwa yamekuzwa shambani kwa gharama finyu, na kisha unachanganya, unaweka kwa sufuria iliyoinjikwa kwa jiko lenye makaa ya moto na unachemsha hadi kuiva.

Kuna kasumba iliyokuwepo katika jamii kwamba katika familia za walimu–hizo ni enzi ambapo taaluma ya ualimu ilikuwa haigusiki kwa kuwa ya hadhi ya juu sana hata pengine kuliko inavyosawiriwa sasa–hazikuwa zikila githeri kwani mshahara ulikuwa ukiwawezesha kulisha familia zao na minofu ya nguvu.

“Kuanzia miaka ya 2000 wakati misimu ya mvua ilianza kuvurugika kutokana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, mazao yalianza kuwa duni na hatimaye janga la njaa likaanza kuwakumba wakulima. Githeri kiligeuka kuwa chakula cha mabwanyenye,” asema Bi Faith Gikunda ambaye ni mshirikishi wa miradi katika shirika la Culture and Ecology (ICE).

Bi Gikunda anasema kwamba janga la njaa kufuatia ukosefu wa mavuno lilipisha biashara kubwa ya uagizaji chakula kilichokuwa kinakuzwa mashambani na hatimaye waliotaka kuendelea kuvuna mahindi na maharagwe pamoja na mimea mingine, ikawabidi kuwekeza vitita vikubwa katika kilimo cha unyunyiziaji mimea maji.

Wengine wanaong’ang’ania kuendelea mbele na kilimo cha nafaka wanajipata wakipambana na kero ya magonjwa ya mimea na wezi kuiba mavuno. Pia kuna hatari ya hali za El-Nino, Lanina na upepo kupindukia bila kusahau kiangazi.

“Wakati ambapo unapata chakula cha jadi katika jamii kimeanza kuwa cha bei ya juu hata kwa wakulima wenyewe, basi elewa umaskini umekita mizizi mashinani,” Bi Gikunda akasema.

Alisema hali hiyo imejiangazia katika jamii zote ambapo si samaki kwa jamii za eneo la Nyanza, si nyama ya mifugo kwa jamii za kuhamahama, si wali kwa watu wa Kirinyaga na Tana River, si muthokoi kwa Wakamba… vyote vimepanda bei.

Hali hii inatokana na gharama za uzalishaji na bei sokoni kupanda kutokana na upungufu na pia ushuru katika biashara.

“Hapo ndipo githeri kilianza kuwa chakula cha hadhi… Miaka ya zamani waliokuwa wakiishi maeneo ya walikuwa wanatamani kusafiri mashinani ndipo wakasherehekee sikukuu kupitia maandalizi ya chapati na wali lakini leo hii wanakimbilia vijijini kula githeri kwa kuwa hali imebadilika,” asema mwenyekiti wa jamii ya Agikuyu Bw Wachira Kiago.

Bw Kiago anasema kwamba familia ambayo leo hii inamudu gharama ya githeri siyo ya kuchezewa kwa kuwa ni ya hadhi.

Kwa mujibu wa Bi Virginia Njeri ambaye huuza nafaka katika soko la Makongo katika viunga vya Mji wa Thika, mahidi kilo moja kwa sasa ni Sh130 huku kilo moja ya maharagwe ikiwa ni Sh200, kumaanisha unahitaji Sh300 kuandaa githeri cha kuliwa na watu watatu ambao si wafakamiaji sana, kwa siku moja.

“Na kumbuka hujahesabu gharama ya makaa, kuni au gesi ikiwa wewe ni mkazi wa mjini. Kuandaa githeri cha watu watatu mjini itakubidi uwe na bajeti isiyopungua Sh400. Ukiamua kukaanga hicho githeri ukizingatia bei ya nyanya, kitunguu na mafuta…ongeza nyama, viazi, mboga…gharama hiyo inaruka hadi Sh800. Ikiwa unataka kuandaa githeri cha kuliwa na familia ya watu watano, basi itabidi uwe na bajeti ya zaidi ya Sh1,600,” asema.

Githeri kikichemshwa kutumia moto wa gesi. PICHA | MWANGI MUIRURI

Wanaotumia njia za mkato ili kujipa mlo wa githeri kupitia kununua kutoka kwa wachuuzi ambao hukipima kwa vikombe mtaani pia wanasema kile cha kiwango cha chini kabisa ambacho huenda kishibishe mtoto pekee, ni cha Sh30.

“Nikitaka githeri mtaani cha kuliwa na familia yangu ya watu sita, labda ninunue cha Sh300… Kwa wachuuzi kunafaa tu kuwa na uteja wa wanaoishi peke yao na ambao hawana majukumu mengi ya kifedha,” akasema Bi Stella Nduku, mkazi wa mjini Thika.

Bi Nduku alisema wengi wanaonelea ni heri kununua chapati mtaani kwa kuwa moja ni kati ya Sh10 na Sh20 na ambapo ukinunua supu ya Sh10 basi maisha yanasonga mbele.

“Hata ile sukumawiki iliyokuwa yasemwa eti husukuma juma kufuatia unyonge wake wa bei sokoni, siku hizi imekuwa tishio kwa wengi kuimudu gharama yake,” aongeza.

Wanaokuwa wabunifu na kuchanganya mahindi na aina ya nafaka kama njahi au njugu ili kuandaa githeri ndio wadosi zaidi kwa kuwa bei itazidi ile ya githeri cha mahindi na maharagwe.

Waziri wa Kilimo na Ustawishaji wa Mifugo Bw Mithika Linturi anasema kwamba anaelewa kuhusu changamoto hiyo.

“Hii ndiyo sababu kwa sasa tunatoa fatalaiza kwa bei nafuu pamoja na kuzidisha kilimo cha unyunyiziaji mimea maji ili turejeshe mavuno kwa mkulima na pia tuzidishe hadi tuwe na ya kushirikisha biashara ili kuwakinga wanaoishi mijini dhidi ya bei za juu kwa chakula,” akasema waziri Linturi.

Bw Linturi alisema ni ukweli kwamba kusambaratika kwa mavuno kumegeuza chakula cha jadi katika jamii kuwa na bei za juu hasa githeri lakini hali hii “tutaibadilisha katika misimu ya hivi karibuni”.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kang’ata afafanua kuhusu waraka uliotangaza...

Polisi wawinda wahalifu waliovamia dukakuu la Shivling

T L