• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Pwani raha yasukuma masponsa kaburini

Pwani raha yasukuma masponsa kaburini

Na BRIAN OCHARO

VIFO vya wazee raia wa kigeni katika maeneo ya Pwani, vinazidi kuibua kiwewe huku baadhi ya kesi zikiendelea kuchukua muda mrefu mahakamani.

Wengi wao waliamua kuweka makao yao Pwani, ila hawakupata nafasi ya kufurahia miaka yao ya uzeeni jinsi walivyotarajia kwani walikutwa na mauti kwa njia za kutatanisha.

Upekuzi uliofanywa na Taifa Leo umegundua kuwa, idadi kubwa ya visa hivyo vinafanana kwa vile vinahusishwa na mizozo ya kimapenzi baina yao na wapenzi walio na umri mdogo mno kuwaliko, huku vingine vikihusu mizozo ya mali na baadhi wakidaiwa kujitoa uhai baada ya kunyonywa mali zao kwa raha za Pwani.

Cha kushangaza ni kuwa wengi wa raia hao wa kigeni kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni kama vile Ulaya, Asia, Uingereza na Amerika hushirikisha wapenzi wao Wakenya katika biashara na wengine wakajenga nyumba za kifahari.

Herman Rouwenhorst, raia wa Uholanzi, ndiye mwathiriwa wa hivi karibuni wa mauaji ya kikatili, ambayo yamehusishwa na utajiri wake mkubwa nchini Kenya na Uholanzi.

MFANYABIASHARA

Rouwenhorst aliyetokea Apeldoorn, Uholanzi, alikuwa mfanyabiashara mahiri, ambaye alikuwa na vilabu vya burudani kadhaa na mali katika kaunti za Mombasa na Kilifi.

Stakabadhi zilizowasilishwa kortini zinaonyesha kuwa Mholanzi huyo alihamia Kenya ili awe karibu na mpenzi wake, Bi Riziki Cherono Ali, ambaye baadaye walioana.

Waliishi pamoja katika nyumba yao mtaa wa Shanzu hadi Juni 4, wakati mwanamume huyo alipokumbana na mauti yake.

Maiti yake ilipatikana nyumbani kwake mnamo Juni 6, 2021, akiwa amefungwa mikono na miguu kwa kamba, na mdomo umezibwa.

Mlinzi wa usiku Evans Bambo Bokolo pia alipatikana ameuawa.Wapelelezi wanamchukulia Bi Cherono, ambaye aliwaarifu polisi kuhusu kisa hicho kama mshukiwa mkuu.

Wengine walioshtakiwa kwa mauaji hayo ni Bw Timothy Omondi Ngowe almaarufu na Bi Mary Nekesa Ambani.

Mwathiriwa mwingine, Krabbe Dieter Gunther, raia wa Ujerumani, ambaye mapema mwaka huu 2021 alipatikana amejitia kitanzi mtaani Bamburi baada ya kudaiwa kumuua mpenzi wake Cynthia Akinyi.

Wawili hao walikuwa wakiishi pamoja mtaa wa Mtwapa, Kaunti ya Kilifi.Polisi walisema Gunther alikuwa akikabiliwa na changamoto za kifedha baada ya kuishiwa na mali alizokuwa nazo.

“Kufikia wakati alipofariki, haikujulikana alikuwa akiishi wapi kwani hakuwa na uwezo wa kulipia kodi ya nyumba wala kununua chakula,” polisi waliohusika katika uchunguzi huo wakasema.

Mnamo Machi 2021, Mjerumani mwingine, Theodore Wolfgang Fischer, alidaiwa kujitoa uhai kwa kujifyatulia risasi nyumbani kwake eneo la Kibundani, Diani, Kaunti ya Kwale.

Wapelelezi walishuku alichukua hatua hiyo baada ya kupoteza pesa na mali kwa marafiki zake, kwani aliacha barua iliyotaja uamuzi wake kujitoa uhai.Ilibainika kuwa, mzee huyo wa miaka 82, ambaye aliishi Diani kwa takriban miaka 30, aliwasilisha barua hiyo kwa Afisa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Diani awali kabla afariki.

“Alilalamikia masuala mbalimbali ikiwemo mizozo ya mali, na jinsi alivyopoteza mali zake kwa watu anaowajua. Mambo haya yalimhangaisha kwa sababu ya umri wake ambao pia ulikuwa ukimdhoofisha kiafya,” maafisa wakasema.

Mwaka 2020, Detering Herman, raia wa Ujerumani, alipatikana amekufa kwa hali ya kutatanisha katika chumba chake mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi.

Kulingana na polisi, mwanamume huyo, 78, alikufa baada ya kuhudhuria shamrashamra za usiku na mpenzi wake.

Ilisemekana msichana huyo alitoweka baada ya kisa hicho.Mnamo Septemba 2017, Mocer Max raia wa Uswisi aliuawa na watu wasiojulikana na mwili wake kutupwa katika Bahari ya Hindi.

Max alikuwa ameishi nchini kwa zaidi ya miaka 10 katika mtaa wa Mtwapa.Mpelelezi ambaye alikuwa akichunguza kisa hicho alisema inashukiwa Max aliuawa kwa sababu ya utajiri wake mwingi.

Mnamo 2016, Jacobus Van Der Goes, raia wa Uholanzi, aliuawa katika hali zisizoeleweka.Akiwa Kenya, mzee huyo, 77, alinunua mali pamoja na nyumba za kifahari katika eneo la Nyali na akamwajiri John Ochieng kama mlinzi wa boma hilo.

Bw Ochieng na mwenzake Joseph Ogolla walihukumiwa kifo na kifungo cha maisha gerezani mtawalia.

Mnamo 2015, mtalii kutoka Italia, Cartei Paolo, 57, alijiua kwa kuruka kutoka jengo la ghorofa nne kwa sababu ya shida za kifedha.

Polisi walisema wakati huo kwamba Paolo hakuweza kumsaidia mkewe na alihamia nyumbani kwa rafiki yake na kwamba biashara kadhaa alizokuwa akifanya zilianguka.

You can share this post!

Wanajeshi kote kote, kulikoni?

Wanajeshi waua waandamanaji 14

T L