• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 AM
Wanajeshi waua waandamanaji 14

Wanajeshi waua waandamanaji 14

Na MASHIRIKA

KHARTOUM, SUDAN

MADAKTARI nchini Sudan wamesema watu 14 waliuawa Jumatano kwa kupigwa risasi na vikosi vya usalama, kwa kufanya maandamano kupinga utawala mpya wa kijeshi.

Madaktari na vyama vya kutetea haki za binadamu walisema idadi hiyo inafikisha jumla ya watu waliouawa tangu mapinduzi hayo kufanyika kuwa 38.

Wanaharakati walikuwa wameitisha maandamano kuadhimisha siku ambapo kiongozi wa kiraia alipaswa kuchukua uongozi wa Baraza Kuu la Utawala, linaloiongoza nchi hiyo.

Baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi mwezi Oktoba, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, aliivunja serikali na kuwakamata mamia ya wanasiasa.

Baadaye, alijitangaza kuwa mkuu wa Baraza Jipya la Utawala.Kumekuwa na hofu kutokana na ukatili ambao vikosi vya usalama vya Sudan vimekuwa vikitumia kuwakabili waandamanaji hao.

Madaktari jijini Khartoum walisema Alhamisi vikosi hivyo vilirusha gesi ya kutoa machozi ndani ya hospitali kadhaa.

Vile vile, wanajeshi wanadaiwa kuwazuia madaktari kuwatibu baadhi ya watu waliojeruhiwa.

Vikosi hivyo pia vimewakamata mamia ya watu katika maeneo yaliyo karibu na jiji hilo.

Serikali pia imezima umeme katika baadhi ya maeneo.

Wanasema lengo la Jenerali Burhan na washirika wake ni kukabili maandamano yoyote dhidi ya utawala kuenea katika maeneo mengine nchini humo.

Waandamanaji walifanya maandamano katika barabara tofauti za mji huo licha ya huduma za simu na intaneti kufungwa na utawala huo.

“Raia waliwachagua uongozi wa kiraia,” wakasema waandamaji hao.

Vile vile, walitoa matamshi ya kumkashifu Jenerali Burhan. Waandamanaji wao, ambapo wengi ni vijana walipiga makofi na kupiga kamsa.

Hata hivyo, ghasia zilizuka baadaye.

Vikosi vya usalama viliwarushia vitoa machozi kwenye juhudi za kujaribu kuwatawanya.

Madaktari hao walisema idadi kubwa ya majeruhi walipigwa risasi vichwani mwao.

Maandamano pia yaliripotiwa kufanyika katika mji wa Port Sudan, kulingana na vyombo vya habari nchini humo.

“Ilikuwa siku mbaya sana kwa waandamanaji,” akasema Soha, aliyekuwa miongoni mwa waandamanaji hao.

“Nilimwona mtu aliyekuwa na majeraha ya risasi akiwa nyuma yangu. Watu wengi sana walikamatwa jijini Khartoum. Madaktari hao walisema watu wengi walijificha kwenye majengo yaliyokuwa karibu, baada ya vikosi hivyo kuwarushia gesi ya kutoa machozi.

Kamati Kuu ya Madaktari nchini humo ilisema vikosi vinawakamata na hata kuwajeruhi watu waliolazwa hospitalini.Chama cha Wataalamu nchini humo pia kimejitokeza kukashifu vikali ukatili huo.

Mnamo Jumatano, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika, Antony Blinken, aliyaomba mataifa ya Afrika kutahadhari vitendo vyovyote ambavyo vinatishia uthabiti wa kidemokrasia.

“Ikiwa jeshi litafuata na kuheshimu taratibu zifaazo kama haki za binadamu, huenda taifa hilo likapata tena uungwaji mkono wa jamii ya kimataifa,” akasema Blinken alipowahutubia wanahabari jijini Nairobi, Kenya.

Kabla ya 2019, Sudan ilikuwa imekumbwa na mapinduzi mengine ya kijeshi.Jenerali Burhan ametangaza hali ya hatari nchini humo.

Licha ya kusisitiza hakuipindua serikali, amekuwa akipata ukosoaji mkubwa kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Naibu Waziri wa Amerika wa Masuala ya Afrika, Molly Phee amekuwa akijaribu kuongoza juhudi za kutafuta amani nchini humo, kwa kuzipatanisha pande zinazozozana.

Phee anautaka utawala huo kumrejesha mamlakani Waziri Mkuu aliyeondolewa mamlakani, Abdalla Hamdok ambaye yuko katika kifungo cha nyumbani.

You can share this post!

Pwani raha yasukuma masponsa kaburini

Kenya yaamua kusubiri Fifa itoe marufuku ya soka nchini

T L