• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 2:24 PM
Wanajeshi kote kote, kulikoni?

Wanajeshi kote kote, kulikoni?

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kujaza wanajeshi katika taasisi muhimu za serikali imeibua maswali huku wadadisi wakihoji lengo lake.

Hii ni baada ya wanajeshi zaidi ya 20 kuteuliwa kushikilia nyadhifa katika taasisi mbalimbali za serikali ndani ya miaka miwili iliyopita.

Brigedia (Mstaafu) John Kibaso Warioba aliyeteuliwa Jumatano kuwa Kamishna wa Magereza, ndiye mwanajeshi wa hivi punde zaidi kutwikwa jukumu la kusimamia taasisi ya umma.

Brigedia (Mstaafu) Warioba alichukua nafasi ya Bw Wycliffe Ogallo aliyetimuliwa baada ya wafungwa watatu wa ugaidi kutoroka kutoka gereza la Kamiti lenye ulinzi mkali.

Wakosoaji wanasema kuwa hatua ya Rais Kenyatta kupenyeza wanajeshi katika taasisi za serikali ni kuhujumu demokrasia.

“Kuteua wanajeshi kuongoza taasisi za kiraia ni pigo kwa demokrasia. Kuondoa aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko, kwa mfano, na kumteua Mohamed Badi, ni tishio kwa demokrasia,” asema Wakili Makau Mutua.

Jenerali Mohamed Badi. PICHA | MAKTABA

Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua pia amekosoa Rais Kenyatta kwa kuteua idadi kubwa ya wanajeshi serikalini akisema: “hivi karibuni tutajipata serikali ikiendeshwa na wanajeshi.”

Rais Kenyatta ametetea uamuzi wake wa kuteua wanajeshi kushikilia nyadhifa serikalini akisema wanaaminika na watamsaidia kuafikia malengo yake ya maendeleo kabla ya kuondoka mamlakani 2022.

“Ni mjinga tu ambaye hataki kutumia watu wanaofanya kazi kwa bidii ili kumsaidia kuafikia malengo yake. Mimi nashirikiana na Wakenya wenye nidhamu na ni wa kutegemewa kuafikia malengo yangu. KDF ni miongoni mwa watu ninaowaamini. Wanajeshi vilevile ni Wakenya sawa na wengine,” Rais Kenyatta amejitetea.

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) pia limeitaka serikali kufanyia mabadiliko na kudhibiti ufujaji wa fedha za umma katika baadhi ya taasisi ili kuwezesha Kenya kupokea mkopo wa Sh256.8 bilioni ulioidhinishwa mapema mwaka huu 2021.

Baadhi ya wataalamu wa masuala ya uchumi wanaamini rais ameamua kuhusisha wanajeshi katika taasisi za kiraia ili kuziba mianya ya ufisadi.

Mdadisi wa masuala ya kisiasa, Ochieng’ Kanyadudi anasema kuwa uteuzi wa wanajeshi unalenga kuleta nidhamu katika taasisi mbalimbali.

“Taasisi nyingi zimejawa na ufisadi. Lakini wanajeshi wana nidhamu ya juu. Wamezoea kufuata maagizo bila kuuliza. Nadhani nidhamu yao ndiyo imefanya Rais Kenyatta kuwaamini,” anasema Bw Kanyadudi.

Wiki iliyopita, Jenerali (Mstaafu) Moses Oyugi aliteuliwa na Waziri wa Michezo Amina Mohamed kwenye kamati ya kusimamia soka baada ya kuvunja Bodi ya Shirikisho la Soka nchini (FKF).

Machi 2020, Rais Kenyatta aliteua Meja Jenerali Mohamed Badi kuongoza Idara ya Huduma jijini Nairobi (NMS). NMS imekuwa ikisimamia huduma za afya, miundomsingi, mazingira, elimu kati ya shughuli nyinginezo.

Katika mwaka wa kwanza, NMS ilitengewa bajeti ya Sh28.3 bilioni – kiasi ambacho kilikuwa karibu maradufu ya Sh15.4 bilioni zilizopewa serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Mnamo Septemba 2020, Rais Uhuru aliagiza Badi kuhudhuria katika Baraza la Mawaziri. Juni 2020, Badi alimteua mwanajeshi mwenzake, Meja Jenerali (Mstaafu) Andrew Ikenye kuongoza bodi ya wakurugenzi wa Kampuni ya Kusambaza Maji Jijini Nairobi.

Wanajeshi wengine sita; Brigedia F. Leuria, Meja J.V Mbithi, Meja A.N Nyakundi, Meja J. K. Ngoroge, Luteni Kanali J.K.Biomdo na Meja A.L. Musoma pia wanafanya kazi katika NMS.

Kanali Alice Mate aliteuliwa miezi sita iliyopita kuwa mkurugenzi Mamlaka ya Kurejesha Mali ya Ufisadi (ARA). Mamlaka hiyo imepewa jukumu la kukabiliana na ufisadi na uhalifu wa ulanguzi wa fedha.

Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Samson Mwathethe sasa ni mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya kuzalisha kawi ya KenGen huku mtangulizi wake, Jenerali (mstaafu) Dkt Julius Karangi akiongoza bodi ya Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF).

Wanajeshi wengine walioteuliwa katika taasisi muhimu za serikali ni Meja Jenerali Omudho Awitta (mwenyekiti bodi ya Shirika la Reli), Brigedia James Githanga (Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Nyama – KMC), Brigedia (mstaafu) John Waweru (Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wanyamapori – KWS), Luteni Kanali (mstaafu) Bernard Njiraini (mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kuhakiki Ubora wa Bidhaa –Kebs), Jenerali (mstaafu) Koseph Kibwana (mwenyekiti wa bodi ya mamlaka ya Bandari – KPA.

You can share this post!

Sitafuti kuwa naibu wa Raila – Kinyanjui

Pwani raha yasukuma masponsa kaburini

T L