• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
TANZIA: MCA wa Chewani aaga dunia baada ya gari lake kugongana na lori kwenye barabara ya Malindi-Garsen

TANZIA: MCA wa Chewani aaga dunia baada ya gari lake kugongana na lori kwenye barabara ya Malindi-Garsen

NA ALEX KALAMA 

MWAKILISHI wa wadi ya Chewani, kaunti ya Tana River Hamisi Idd Deye, ameaga dunia baada ya kuhusika katika ajali iliyotokea eneo la Kanagoni, Kaunti ya Kilifi, kwenye barabara kuu ya Malindi-Lamu.

Hamisi alikuwa MCA ambaye alikuwa ameanza kuhudumu muhula wake wa kwanza katika nafasi hiyo ya uongozi baada ya kuchaguliwa kwa tiketi ya chama cha UDA kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Awali kiongozi huyo alikuwa mlizi wa Gavana wa Kaunti ya Tana River Dhadho Godana katika awamu ya kwanza ya uongozi wake.

Bw Deye alikuwa safarini akitoka mjini Hola akielekea Malindi pale gari lake liligongana na lori la mizigo.

Marehemu Hamisi Idd Deye, MCA wa Chewani amefariki baada ya gari lake kugongana na lori kwenye barabara ya Malindi-Garsen mnamo Juni 17, 2023. PICHA | STEPHEN ODUOR

Kulingana na polisi, gari hilo lilikuwa likiendeshwa kwa kasi, na hivyo dereva wake akashindwa kudhibiti mwendo wake.

Diwani ameaga dunia kwenye sehemu ya tukio hilo huku dereva wake akipata majeraha mabaya.

Akithibitisha ajali hiyo, kamanda wa polisi wa eneobunge la Magarini Daniel Kimbio amesema kuwa ajali hiyo imehusisha gari dogo la kiongozi huyo na lori la mizigo wakati gari hilo dogo lilipojaribu kulipita lori hilo kabla ya kupoteza mwelekeo na kugongana.

Aidha Kimbio amedokeza kuwa dereva wa MCA huyo ameponea chupuchupu huku watu waliokuwa katika lori nao wakipata majeraha madogo madogo.

Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na mwakilishi wa wadi ya Garsen ya Kati Masha Boru na mwakilishi wadi ya Kipini Mashariki Musa Wario, wameelezea kusikitishwa na kutokea kwa ajali hiyo huku wakieleza kuwa kifo cha kiongozi huyo ni pigo kwa kaunti hiyo.

Mwili wa marehemu Deye umepelekwa  katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Star.

  • Tags

You can share this post!

Leicester City waajiri kocha Enzo Maresca

Giroud na Mbappe wabeba Ufaransa dhidi ya Gibraltar kwenye...

T L