• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:01 PM
Leicester City waajiri kocha Enzo Maresca

Leicester City waajiri kocha Enzo Maresca

Na MASHIRIKA

LEICESTER City wameajiri aliyekuwa kocha msaidizi wa Manchester City, Enzo Maresca, kuwa kocha wao mpya hadi mwaka wa 2026.

Maresca, 43, anaingia rasmi kambini mwa Leicester siku sita baada ya Man-City kunyanyua ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na kukamilisha kampeni za msimu wa 2022-23 wakijivunia jumla ya mataji matatu.

Mkufunzi huyo raia wa Italia anajaza pengo la kocha mshikilizi Dean Smith aliyeongoza Leicester kushinda mechi mbili pekee kati ya nane. Msusuru huo wa matokeo duni ulichangia kuteremshwa ngazi kwa Leicester kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mimuu.

Leicester pia wamethibitisha kwamba hawatarefusha mkataba wa Smith utakapokamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Juni huku waliokuwa wasaidizi wake Craig Shakespeare na John Terry pia wakiondoka.

Kwa kujiunga na Leicester, Maresca anatamatisha kipindi cha kuwa sehemu ya benchi ya kiufundi ya kocha Pep Guardiola aliyeanza kumkumbatia kama msaidizi wake katika kikosi cha kwanza cha Man-City miaka miwili iliyopita baada ya kuhudumu katika kikosi cha chipukizi wa U-23.

Aliwahi kuhudumu kambini mwa Parma kwa siku 180 akiwa kocha mnamo 2021, ambapo aliongoza kikosi hicho kushinda mechi nne pekee kutokana na 14 baada ya kuteremshwa ngazi kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Leicester wamerejea tena kwenye ligi ndogo ya Championship kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 10 baada ya matokeo duni katika EPL msimu huu, ambapo waliambulia nafasi ya 18 jedwalini kwa kushinda mechi tisa pekee.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Paka mweusi amzuia jamaa aliyejaribu kuondoka dukani bila...

TANZIA: MCA wa Chewani aaga dunia baada ya gari lake...

T L