• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Ukimwi: Wajawazito Kilifi washauriwa kuhudhuria kliniki kuzuia maambukizi ya mama hadi kwa mtoto

Ukimwi: Wajawazito Kilifi washauriwa kuhudhuria kliniki kuzuia maambukizi ya mama hadi kwa mtoto

NA ALEX KALAMA 

MAAMBUKIZI ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama hadi mtoto, haswa akina mama wajawazito na hata wanaonyonyesha yameongezeka katika siku za hivi karibuni ndani ya Kaunti ya Kilifi.

Kwa mujibu wa idara ya afya katika Kaunti ya Kilifi, kuanzia Januari hadi Juni, watoto 33 wameambukizwa virusi hivyo na akina mama zao kutokana na akina mama hao kugomea kuenda kliniki kufanyiwa uchunguzi wa kiafya, huku wengine wakigomea kutumia dawa za kumlinda mtoto aliye tumboni, hali ambayo wataalamu wanasema inafaa kushughulikiwa kwa haraka kabla ya kitumbua kuingia mchanga.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo msimamizi wa kitengo cha kufuatilia na kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto ndani ya Kaunti ya Kilifi Bi Gladys Sitemesi ameeleza kuwa kumerekodiwa kuongezeka kwa maambukizi mapya ya virusi haswa baada ya taifa kufaulu kupambana na corona.

“Walikuwa wanasema mwaka 2022 Kilifi ni mojawapo ya zile kaunti ambazo zimeongeza maambukizi mapya na tukapinga. Lakini jinsi siku zinavyoendelea kusonga tumeona kwamba maambukizi mapya yanaendelea kuongezeka. Ukiangalia matumizi ya PrEP katika kaunti hii ni ya kiwango cha chini mno, jambo ambalo pia limechangia visa hivi vipya,” alisema Bi Sitemesi.

Kulingana na msimamizi huyo, akina mama wengi wanaopatikana kuwa na virusi na hata kuambukiza wana wao ni wale wenye umri wa chini ya miaka 24, hali inayotokana na akina mama hao kususia kwenda kliniki.

“Mtu anaona bado ni mdogo kiumri hawezi kwenda kliniki… na hao ndio unapata mara nyingi wataambukiza watoto wao endapo wana virusi vya Ukimwi kwa maana wanakosa dawa yoyote ya kuzuia makali,” alisema Bi Sitemesi.

Wakati huo huo mshirikishi wa afya ya uzazi Kaunti ya Kilifi Kenneth Miriti ameeleza kuwa kando na maambukizi ya virusi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto, kumekuwepo na maambukizi mapya miongoni mwa jamii.

“Tulikuwa mahali ambapo unyanyapaa ulikuwa umepungua… hapo ni kabla ya corona. Lakini baada ya kuwa tumetoka kwa janga la Covid -19 unyanyapaa wa walioambukizwa virusi vya Ukimwi umepanda sana, na maambukizi mapya pia yamepanda sana. Kilifi peke yake ukiangalia sasa hivi tuko na watoto zaidi ya 30 ambao wameambukizwa virusi. Hii inamaanisha hizo ni familia zaidi ya 30… na hii ni kutoka kwa mama hadi mtoto. Kwa hivyo kuna haja ya kufanya hamasisho ili kuzuia hali isiwe mbaya zaidi,” alisema Bw Miriti.

  • Tags

You can share this post!

Wanariadha maarufu wa kikosi cha Marathon wajiondoa Team...

Mkazi wa jiji anyakwa akilalama

T L