• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Wachimbaji madini waandamana kushinikiza mgodi ufunguliwe

Wachimbaji madini waandamana kushinikiza mgodi ufunguliwe

NA LUCY MKANYIKA

WACHIMBAJI madini aina ya quartz eneo la Kishushe katika Kaunti ya Taita Taveta wamekuwa wakipiga kambi katika kituo cha polisi cha eneo hilo ili kushinikiza kufunguliwa kwa mgodi wao.

Kwa siku mbili mfululizo, Alhamisi na Ijumaa, wachimbaji hao wa madini hayo walionekana katika kituo hicho wakiitaka serikali kuachilia malori mawili yaliyozuiliwa na polisi wa eneo hilo.

Mnamo Alhamisi, polisi wakiongozwa na mkuu wa kaunti ndogo ya Wundanyi Bw Maina Ngunyi walizuia wachimbaji hao wadogowadogo kusafirisha madini hayo kutokana na utata baina ya makundi mawili.

Polisi wakizuia malori ya madini. PICHA | LUCY MKANYIKA

Bw Ngunyi alitoa amri hiyo baada ya madai kuwa ranchi ya Kishushe ilitoa kibali cha uchimbaji kwa makundi mawili swala ambalo limepingwa na usimamizi.

Hata hivyo wachimbaji hao walidai kuwa kundi moja linalodai kumiliki sehemu hiyo lilijeruhi dereva mmoja wiki iliyopita.

Dereva huyo aliyekuwa akisafirisha madini hayo alijeruhiwa katika eneo la Mbulia katika barabara ya Kishushe/Ndii.

“Badala ya serikali kuchukulia hatua wahalifu hao inakuja kutufungia mgodi ambao tunautegemea kulisha familia zetu,” akasema Bw Albert Mwatiriri.

Hata hivyo, Bw Ngunyi alisema kuwa serikali ilichukua hatua hiyo ili kuzuia maafa zaidi.

“Tumetoa amri ya kusimamisha shughuli zote za uchimbaji katika mgodi huu hadi pale makundi haya yatakaposikilizana,” akasema.

Aidha, alidai kuwa kundi la Ngolia B ambalo linazozana na lile na Mwarangenyi halina leseni ya uchimbaji kutoka kwa Wizara ya Madini.

“Kuna afisi husika na ninaomba vikundi hivi kuungana ili kujua jinsi ya kupata idhini ya uchimbaji,” akasema.

Usimamizi wa ranchi hiyo ya Kishushe ambao uliwakilishwa na Bi Matilda Waleghwa umekana kutoa idhini ya uchimbaji kwa kikundi cha Mwarangenyi.

Bi Waleghwa alidai kuwa baadhi ya maafisa wa serikali wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya viongozi wa eneo hilo kukandamiza wachimbaji wadogowadogo.

“Kwa nini watu wengine wanaruhusiwa kusafirisha madini huku hawa wadogowadogo wakizuiliwa? Hatutakubali kamwe ugandamizaji wa aina hii,” akasema.

Alisema kuwa ranchi hiyo imetoa kibali kwa makundi 23 ya wachimbaji wadogowadogo huku akiitaka serikali kuondoa vikwazo ili wenyeji wanufaike kutokana na madini yaliyoko katika eneo hilo.

Kijana mmoja wa eneo la Kishushe Bw Meshach Mati alisikitikia hatua ya kufungwa kwa mgodi huo ambao alisema umetoa ajira kwa vijana wengi wa eneo hilo.

“Ukosefu wa ajira nchini umekuwa changamoto kwa vijana wengi. Licha ya kuwa tumepata ajira ni swala la kuvunja moyo kuona kuwa asasi za serikali yetu zinatumiwa kutukandamiza,” akasema.

Eneo la Kishushe linajulikana kwa madini ya aina mbalimbali yakiwemo yale ya chuma.

Licha ya hivyo, wenyeji wangali wakiishi katika hali ya umaskini huku madini hayo yakifaidi wawekezaji na watu wachache wa eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

Matumizi ya kiholela ya dawa za kupunguza maumivu ni hatari

Olimpiki Maalum: Lynette Gitimu na Abigail Njuguna wavunia...

T L