• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 4:32 PM
Wakazi walilia Rais Ruto anunue ardhi ili wasifurushwe

Wakazi walilia Rais Ruto anunue ardhi ili wasifurushwe

NA JURGEN NAMBEKA

WAKAZI wa Soweto, eneobunge la Nyali Kaunti ya Mombasa, wanaoishi kwa ardhi ya ekari 13 iliyokuwa ikizozaniwa kwa muda, wamemtaka Rais William Ruto na mbunge wao Mohamed Ali kuingilia kati ili wasifurushwe.

Mahakama ilikuwa imewapa wakazi hao siku 30 kuondoka kwenye ardhi hiyo, baada ya mmiliki wa ardhi hiyo Bw Mohamed Hatimi kushinda kesi.

Kulingana nao, walikuwa wameishi katika ardhi hiyo kwa muda mrefu.

Walieleza kuwa kubomolewa kwa mali yao huenda kukawapa hasara na kuwaacha katika njia panda.

Mmoja wa wakazi wa ardhi hiyo Bw Liverson Mkala, ambaye ameishi katika shamba hilo kuanzia 1989, alieleza kuwa msukumo baina ya mmiliki na wakazi ulianza mwaka 2006.

“Tumebomolewa sehemu hii karibu mara tano. Hapa tunaishi zaidi ya familia 260. Wazee, akina mama na watoto. Kutufurusha kutatuacha katika njia panda kwa kuwa hatujui tuednde wapi,” akasema Bw Mkala.

Mkala anasema aliingia katika ardhi hiyo wakati ambao haukuwa na ua.

Rais Ruto wiki jana katika ziara yake Pwani, alisisitiza kuwa serikali yake ilikuwa na nia ya kununua ardhi zinazomilikiwa na watu wasiokuwepo, ili kuwapa maskwota makazi.

“Tumetenga Sh1 bilioni kulipa wamiliki wasiokuwepo na kuwapa watu wetu ardhi ili wasiishi kama maskwota,” akasema Dkt Ruto.

Mkazi wa miaka 13 Bi Ruth wanjiru, anaeleza kuwa alipoingia eneo hilo hakuwa anafahamu ardhi hiyo ilikuwa na utata hadi alipoitwa mahakamani.

“Nilipokaribishwa katika eneo hili na marafiki na majirani sikujua kulikuwa na mzozo wa ardhi. Tulipata tu tukiitwa mahakamani na ikabidi kama wakazi tutafute wakili. Ila sasa kesi ilikamilika na tukaambiwa tuondoka ndani ya siku 30. Sasa ni siku 27,” akasema Bi Wanjiru.

Kulingana naye, hata mwanawe alikuwa ameomba mkopo na kujenga nyumba yake, ila sasa kuna uwezekano wa kupoteza mali yao yote.

“Tunaomba Rais, Gavana Abdulswammad Nassir, mbunge wetu Ali, watutetee kwa kuwa mimi kama mjane pesa zote nilizokuwa nazo niliwekeza katika nyumba. Nitaenda wapi,” akasema Bi Wanjiru.

Eneo hilo lina shule, makanisa, misikiti, shule za kidini nyumba za kupanga na za kibinafsi.

“Imebaki siku kadhaa tuvunjiwe na roho zetu zi mikononi, tunaomba viongozi wetu waingilie kati tupate suluhisho tusifurushwe wala kuvunjiwa,” akasema Bw Ala Min.

 

  • Tags

You can share this post!

Serikali yamjengea chifu wa Bondo aliyechomewa nyumba...

Jamii yaambiwa ndoa za wake wengi huwaweka wanawake kwa...

T L