• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Jamii yaambiwa ndoa za wake wengi huwaweka wanawake kwa hatari ya kansa ya mlango wa kizazi

Jamii yaambiwa ndoa za wake wengi huwaweka wanawake kwa hatari ya kansa ya mlango wa kizazi

NA KALUME KAZUNGU

KANSA ya mlango wa kizazi inazidi kuathiri wanawake wengi katika Kaunti ya Lamu ambao sasa wanawanyooshea kidole cha lawama waume wao kwa kuwa na macho ya nje.

Pia, wataalamu wamesema, ndoa za mume kuwa na wake wengi huchangia hali hii.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili, baadhi ya wanawake walilakamika kuwa waume wengi wametumia mwanya wa mafundisho ya kidini kuendeleza hulka ya mipango ya kando, hali ambayo wanahisi ni changizo kuu ya wanawake hao kupata kansa ya mlango au shingo ya kizazi.

Afisa Mshirikishi wa Masuala ya Afya ya Uzazi,Kaunti ya Lamu, Bi Fatma Faruk alikiri kuwa visa vya saratani ya shingo ya kizazi vimeongezeka miongoni mwa wanawake, akisisitiza haja ya wanandoa kuwa waaminifu na wapenzi wao.

Ripoti ya hivi majuzi ya Idara ya Afya,kaunti ya Lamu inaashiria kuwa karibu visa kumi vya kansa hugunduliwa eneo hilo kila mwaka, idadi kubwa ya visa hivyo ikiwa ni ile ya saratani ya shingo ya kizazi.

Ikumbukwe kuwa saratani ya shingo ya kizazi inaweza kutibika kwa urahisi iwapo itagundulika mapema.

Bi Faruk aidha alitaja kutokuwepo kwa ufahamu na ujuzi kati ya wanawake, ambao husababisha hatari kali zaidi au matatizo ya ugonjwa huu.

Bi Fatma Faruk (mbele) akiwa na maafisa wengine wa afya wakati wa hamasisho kuhusu kansa kisiwani Lamu. Kukithiri kwa kansa ya mlango wa kizazi kwahofisha wakazi na wataalamu wa afya. PICHA | KALUME KAZUNGU

Miongoni mwa dalili za kuugua kansa ya shingo ya kizazi ni kumwagika kati ya vipindi, hasa inapoonekana kila baada ya tendo la ndoa, harufu mbaya, damu baada ya wanawake kupitisha umri wa kutoka damu ya kila mwezi yaani menopause.

Kulingana na maelezo yasayansi na matibabu, saratani ya shingo ya kizazi husababishwa na ukuaji usiodhibitiwa wa seli kwenye mlango au mdomo wa uterasi. Katika asilimia 99 ya visa, Virusi vya Papilloma ya Binadamu (HPV) vimegunduliwa kuwa kisababishi cha magonjwa ya zinaa hadi kwenye kizazi.

Ikumbukwe kuwa kuna takriban aina 100 za HPVs. Kati ya hizo 16 au 18 zinajulikana kwa kusababisha saratani ya shingo ya kizazi.

Mara nyingi, virusi hujiondoa vyenyewe, lakini kwa asilimia ndogo, kati ya 1 na 2 ya watu, huendelea kusababisha saratani.

“Ni wazi kwamba saratani,hasa ile ya shingo ya kizazi hapa Lamu ipo na inasumbua wanawake wengi. Baadhi ya visababishi ni wapenzi kutokuwa waaminifu kwa ndoa. Utapata mume akijihusisha na wapenzi wengi, hivyo kuishia kusambazia Yule aliye mkewe virusi vya HPV ambavyo ndivyo vinavyochangia kansa ya shingo ya kizazi. Ningeshauri,iwe ni wanaume au wanawake wazidishe uaminifu ndoani. Tudumishe wapenzi wetu. Ikiwa wewe Ni mume Wa mke mmoja basi dhibiti hiyo hali. Na wanawake nao tudumishe wapenzi wetu badala ya kujihusisha kingono Na waume wengi,hivyo kujihatarisha wewe mwenyewe kuugua kansa ya mlango wa kizazi,” akasema Bi Faruk.

Afisa huyo aliwashauri akina mama, Kaunti ya Lamu kuwa na hulka ya kutembelea vituo vya matibabu, ikiwemo hospitali na zahanati ili kukaguliwa na iwapo wana saratani ya shingo ya kizazi basi idhibitiwe Mapema badala ya kuishi gizani na kujipata ukiugua ugonjwa huo katika awamu ngumu isiyoweza kudhibitiwa.

“Wanawake wengi hapa Lamu hawajajitolea kugakuliwa na kupimwa kansa, iwe ni ya mlango wa kizazi au hata ile ya matiti. Ningewasihi wanawake wenzangu mjitolee kupimwa hiyo kansa ya shingo ya kizazi ili iwapo tutapatikana nayo basi ishyghulikiwe mapema kimatibabu,” akasema Bi Faruk.

Bi Khadija Mohamed, mmoja wa wanaharakati wa kijamii kaunti ya Lamu, alisema wakati umewadia kwa wanaume,hasa wale wa dini ya Kiislamu kufikiria juu ya ndoa zao na kuzingatia kumudu ndoa ya mke mmoja Kwa manufaa ya afya ya wapenzi wao.

“Najua leo hii kumshauri mwanamume,hasa Muislamu kuwa na mpenzi au mke mmoja ni ngumu lakini wakati uliopo sasa lazima tulitafakari na kulizingatia kwa dhati suala Hilo. Ni wazi chovyachonya ya wanaume hapa na pale kingono inachangia hiyo saratani ya shingo ya kizazi,hasa kwetu sisi wanawake. Ikiwa waume wetu wanatupenda kweli basi wanawazia hili Kwa manufaa ya afya na hata familia zetu,” akasema Bi Mohamed.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Kaunti ya Lamu, Dkt Mbarak Bahjaj alisema kutokana na mzigo wa wagonjwa wa kansa Lamu kila mara kupewa rufaa ya matibabu kaunti ya Mombasa, ambapo inakuwa ghali kwao, serikali ya kaunti iko mbioni kuanzisha kituo cha ukaguzi, matibabu na uuguzi wa saratani eneo hilo.

Alisema tayari Sh50 milioni zimetengwa kuanzisha mradi huo huku akikadiria kima cha Sh200 milioni zinazohitajika kukamilisha na kufungua rasmi kituo hicho.

“Tunakubali kabisa kwamba Lamu tuko na changamoto ya kukithiri kwa visa vya kansa miongoni mwa wakazi. Karibu kila mwaka hatukosi visa vinavyobainishwa 10 vya watu kuugua saratani aina mbalimbali eneo hili. Tayari tumepeleka visa 10 vya watu kuugua kansa hapa Lamu katika hospitali ya Coast General huko Mombasa kwani hapa hatuna kitengo chochote cha kushughulikia wagonjwa wa kansa. Tumetenga Sh50 milioni kuanzisha kitengo hicho ili kupunguza gharama kwa familia za wagonjwa wa kansa kutafuta matibabu maeneo ya mbali,” akasema Dkt Bahjaj.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi walilia Rais Ruto anunue ardhi ili wasifurushwe

Naibu Rais asifia juhudi za Ruto kujitolea kuwekeza katika...

T L