• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:55 AM
Wakazi washinikiza ajali za ndege zinazojirudia uwanjani Kiunga zichunguzwe

Wakazi washinikiza ajali za ndege zinazojirudia uwanjani Kiunga zichunguzwe

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa Kiunga sasa wanaishinikiza serikali kupitia kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini Kenya (KCAA) kwa ushirikiano na Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini (KAA) kufanya uchunguzi wa kina, hasa kuhusiana na kujirudiarudia kwa ajali eneo hilo.

Kilio chao kinakuja siku moja baada ya kutokea kwa ajali ya ndege iliyowaacha maafisa 10 wakiwemo wanajeshi saba, polisi, rubani na msaidizi wake wakijeruhiwa mjini Kiunga mpakani mwa Kenya na Somalia.

Si mara ya kwanza ndege kugonga mlingoti na nyaya za stima na kusababisha ajali kwenye kiwanja hicho kidogo cha ndege cha Kiunga.

Wakizungumza na Taifa Leo Jumatatu, wakazi walihofia huenda kuna hitilafu ya kimiundomsingi kwenye kiwanja hicho cha ndege ambayo iwapo haitashughulikiwa na kurekebishwa mapema huenda ikasababisha maafa makubwa, si kwa wanaopaa au kutua na ndege tu bali pia kwa wakazi au jamii yote inayoishi au kupakana na kiwanja hicho.

Bw Mohamed Kupi, mkazi wa mji wa Kiunga, alieleza tukio la Jumapili la ajali ya ndege hiyo ndogo kuwa la kutisha na ambalo lazima lishughulikiwe na kutatuliwa vilivyo.

Wakati wa ajali hiyo ya saa saba mchana, nyumba moja iliyokaribiana na pahali ambapo ndege ilianguka na kulipuka ilichomeka pamoja na mali ya thamani isiyojulikana iliyokuwa ndani ya nyumba hiyo.

“Lazima hizi ajali za ndege kwenye kiwanja chetu kidogo cha Kiunga zichunguzwe. Itakuwaje kila wakati ndege inapaa au kutua na kisha kugonga mlingoti na nyaya za stima na kuhatarisha maisha ya wasafiri na sisi wenyeji hapa?Ni wakati wa serikali kupitia KCAA na KAA kuja pamoja kujadili ni nini hasa kipasacho kufanywa hapa. Hali ikiendelea hivi huenda tukashuhudia ajali mbaya zaidi na maafa mengi hapa,” akasema Bw Kupi.

Bi Rukia Ali,mkazi wa Kiunga, alisema lazima kuna kasoro inayopaswa kurekebishwa uwanjani Kiunga.

“Serikali, KCAA, na KAA waje kujadili, kuchunguza na kubaini kiini cha hizi ajali. Kama uwanja wa ndege upo mahali pasipofaa uhamishwe. Ikiwa pia milingoti ya stima iliyoko karibu na kiwanja cha ndege cha Kiunga haipaswi kuwepo basi ing’olewe na kuwekwa eneo la mbali na ambalo ni salama kwa wale wanaoingia na kutoka uwanja mdogo wa ndege wa Kiunga. Hatupendezwi na hizi ajali za kujirudiarudia na zinazofanana kila mara,” akasema Bi Ali.

Wakazi pia waliiomba serikali kumfidia mwaathiriwa ambaye nyumba yake na mali viliteketea kwenye ajali ya ndege iliyotokea Jumapili.

“Tunafahamu kuwa ndege iliyoanguka ni ya serikali. Ni vyema hii familia iliyoachwa ikikaangwa na kijibaridi usiku kucha baada ya nyumba yao kuungua ifidiwe. Hakuna kilichookolewa kwenye nyumba hiyo kwani moto ulikuwa mkali,” akasema Bw Ahmed Bahero.

Mbali na ajali ya Jumapili ambapo ndege ndogo ya serikali aina ya 5Y-GOK Cesna 208 ilianguka baada ya kugonga mlingoti na nyaya za umeme, ajali nyingine sawa na hiyo ni ile ya Juni 2020 ambapo ndege nyingine ya kibinafsi iliyokuwa imesafirisha shehena ya miraa kutoka Isiolo kuja Lamu ilianguka wakati ikitua kwenye uwanja huo mdogo wa Kiunga.

Ajali hiyo pia ilisababishwa na ndege husika kugonga mlingoti wa stima na kuanguka.

Hata hivyo rubani wa ndege hiyo aliyekuwa ndani alinusurika bila majeraha yoyote.

  • Tags

You can share this post!

Mwitaliano apokonya Mkenya Chager ubingwa EA Safari Classic

KWPL kuchukua mapumziko mafupi warembo wapunge unyunyu...

T L