• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Wito jamii ishughulikie afya ya akili visa vya watu kujiua vikiongezeka Siaya

Wito jamii ishughulikie afya ya akili visa vya watu kujiua vikiongezeka Siaya

NA KASSIM ADINASI

WAKATI Kenya iliungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Kuzuia Visa vya Watu Kujitoa Uhai mnamo Jumapili, Septemba 10, 2023, hofu imezuka kwamba idadi ya watu wanaojitoa uhai katika Kaunti ya Siaya inazidi kupanda.

Kamanda wa Polisi wa Siaya Michael Muchiri alisema kwa takriban visa 39 vya watu kujitoa uhai katika kaunti hiyo kati ya Septemba 2022 na Septemba 2023, wanaume ni 32, wanawake ni watatu nao wanne wakiwa ni watoto wa umri wa kati ya miaka minane na 12.

“Hivi visa vya watu kujiua vinatokana na tatizo la afya ya akili linalozidi kuwa pasua kichwa, baadhi ya visababishi vikiwa ni matumizi ya dawa za kulevya, changamoto na kifedha na ugumu wa maisha na migogoro ya kifamilia ikiwemo mizozo ya mashamba,” akasema Bw Muchiri.

Siaya imekuwa ikigonga vichwa vya vyombo vya habari kwa suala la watu kujitoa uhai.

Mnamo Julai 7, 2023, polisi wa kituo cha polisi cha Bondo, Michael Kyalo, alimpiga mkewe kwa risasi kabla ya yeye kujiua kwa risasi vilevile.

 “Kitu saa bili na dakika 35 asubuhi, polisi Michael Kyalo aliyekuwa na bunduki aina ya AK yenye nambari ya utambulisho ya 5524195 alimpiga risasi mkewe kwa jina Brenda Kangai Kimanzikwa paja lake la kushoto na kisha naye akajifyatulia risasi,” ripoti ya polisi ikasema.

Mke huyo alifariki siku chache baadaye.

“Afisa huyo alijipiga risasi chini ya taya ikatokea kichwani na akafa papo hapo,”ripoti ya polisi ikasema mnamo Julai 7.

Ilidaiwa kwamba afisa na mkewe walikuwa na tofauti za kinyumbani.

Kamanda wa polisi wa Bondo Ibrahim Kosi alimrejelea polisi aliyetekeleza kitendo hicho kwamba kwa maisha yake ya kawaida alionekana mtu mtulivu.

“Polisi huyo alikuwa mtu mtulivu. Asubuhi alikuwa ameenda kudumisha usalama katika mahakama kabla ya kurudi nyumbani ambapo alitofautiana na mkewe na akachukua hatua hiyo. Tumeanzisha uchunguzi,” akasema Bw Kosi.

Na miezi mitatu kabla ya kisa hicho, afisa wa kituo cha polisi cha Siaya Kaduol katika eneobunge la Gem alijipiga risasi na akafariki papo hapo. Konstebo Maurice Chillison Kisiagi alitumia bunduki yake ya kazi kujiua.

“Polisi huyo alikuwa amehudumu katika kituo hicho kwa mwezi mmoja baada ya kuhamishiwa hapo akitokea Kisumu mwezi wa Februari 2023,” Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Gem Cecilia Kemboi aliambia wanahabari.

Aprili 2023, kisa kingine kiliripotiwa ambapo katika kijiji cha Obaga kilichoko Sakwa Kusini katika kaunti ndogo ya Bondo mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza aliyekuwa na umri wa miaka 18, alijiua. Mwili wa David Okoth Otieno aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Orengo ulipatikana ukining’inia juu mtini. Chifu wa kata ya Nyaguda, Bw Collins Abuto, alisema wanakijiji ndio waliowafahamisha polisi kuhusu mkasa huo.

Kamanda wa Polisi wa Siaya anafafanua zaidi kuhusu takwimu za watu kujitoa uhai.

“Takwimu zinaonyesha idadi ya wanaume ni asilimia 82, wakifuatwa na watoto kwa asilimia 10 nayo idadi ya wanawake wanaojitoa uhai ikiwa ni asilimia nane,” akasema Bw Muchiri anayependekeza kwamba wadau wote katika jamii yakiwemo makundi ya kidini, serikali, viongozi na wataalamu wa masuala ya afya ya akili wanafaa kutafuta suluhu kumaliza zimwi hili.

Naye mwanaharakati Shirleen Otieno, anasema ni sharti mada hii ya watu kujitoa uhai ipewe kipaumbele na walio kwa uwezekano mkubwa wa kuchukua hatua hii ya kusikitisha wanafaa kuongeleshwa na kupewa mawaidha ya namna ya kukabili changamoto maishani na kurudisha hali ya kawaida.

  • Tags

You can share this post!

IDPs 200,000 walioachwa nje ya mpango wa ridhaa wataka Rais...

Jamii yashtuka radi kupiga na kuua mke na mume, kujeruhi...

T L