• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Rais Ruto: Pasta MacKenzie ni mhalifu anayepaswa kuwa jela

Rais Ruto: Pasta MacKenzie ni mhalifu anayepaswa kuwa jela

Na SAMMY WAWERU

RAIS William Ruto amevunja kimya chake kuhusu mchungaji tata Paul MacKenzie, akisema pasta huyo ni mhalifu anayepaswa kuwa jela.

Kulingana na kiongozi wa nchi, Bw MacKenzie hana tofauti na mhalifu ambaye makao yake ni jela.

Kufuatia visa vya maafa vilivyoandikishwa Kilifi vinavyohusishwa na mhubiri huyo, Dkt Ruto alitangaza Jumatatu kwamba ameamuru asasi za uchunguzi kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika na kumchukulia hatua kali kisheria.

“Mackenzie ni sawa na mhalifu. Hana tofauti na wahalifu wanaopokonya watu nafsi zao,” alisema Rais.

Alitoa matamshi wakati akihutubu katika hafla ya kufuzu kwa makuruti wa askarijela, Chuo cha Mafunzo Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Mchungaji huyo ambaye ni mwasisi wa Kanisa la Good News International, analaumiwa kwa kuhadaa wafuasi wake kufunga bila kula wala kunywa, akiwaahidi kuwa wakifa wataweza kuuridhi Ufalme wa Mungu na pia kukutana na Yesu.

Hadaa za dhehebu lake potovu, limesababisha vifo vya wafuasi wengi kufikia Jumatatu mchana miili 42 ikiandikisha kufukuliwa kwenye makaburi yaliyoko katika shamba lake la ekari 800 Msitu Shakahola, Malindi.

Mhubiri Paul Mackenzie baada ya kuachiliwa na Mahakama Kuu ya Malindi. PICHA | HISANI

Kwa mujibu wa miili iliyofukuliwa na wafuasi waliookolewa, wanawake na watoto ndio waathiriwa wakuu.

Akitoa onyo kali kwa viongozi wa kidini sampuli ya Pasta MacKenzie, Rais Ruto pia alisema ameagiza asasi za usalama kuzima makanisa ya aina hiyo na maeneo ya kuabudu yanayohadaa waumini.

“Kanisa au dhehebu lolote linalohubiri watu wasipate matibabu na dhidi ya kuenda shule, hatua kali kisheria zitachukuliwa.”

Akaongeza: “Madhehebu ya aina hiyo lazima yafungwe. Hatutaruhusu mahubiri ya uongo na hadaa zinazosababisha maafa.”

Akikashifu vikali kitendo cha MacKenzie, Dkt Ruto alisema mchungaji huyo hapaswi kudai ni wa dini ilhali tabia zake ni mbovu.

Pasta huyo amezuiliwa na polisi, huku Idara ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI) ikiendeleza uchunguzi ili kumfungulia mashtaka.

  • Tags

You can share this post!

Azimio kurejelea maandamano jijini Nairobi

IG Koome afika Shakahola idadi ya walioangamia ikigonga 50

T L