• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Ajali: Wawili waokolewa mawimbi yakitatiza utafutaji wa nahodha wa boti

Ajali: Wawili waokolewa mawimbi yakitatiza utafutaji wa nahodha wa boti

NA KALUME KAZUNGU

WATU wawili wameokolewa huku mmoja juhudi za kumtafuta nahodha zikiendelea baada ya boti walimokuwa wakisafiria kuzama katika kivuko cha Shee-Mwanasha, eneo la Mkokoni, tarafa ya Kiunga, Lamu Mashariki leo Ijumaa.

Boti hiyo ilikuwa ikisafirisha miraa kutoka jeti ya Mokowe, Lamu Magharibi kuelekea Kiunga mpakani mwa Lamu na Somalia kabla ya kusombwa na mawimbi makali na kuzama.

Jumla ya watu watatu, akiwemo nahodha wa boti hiyo na wasaidizi wake wawili walikuwa ndani ya boti hiyo wakati ajali ilitokea.

Aliyepotea ni nahodha wa boti hiyo.

Boti na miraa iliyokuwa imebebwa pia haijapatikana. Ilikuwa imebeba magunia 15 ya miraa.

Afisa anayeongoza wapiga-mbizi wa kujitolea mhanga, Mohamed Athman Mote, amesema shughuli za kusaka aliyepotea na boti zinatatizwa na mawimbi makali yanayoshuhudiwa kwenye kivuko cha Shee-Mwanasha.

Boti hiyo ilizama majira ya saa tano asubuhi.

“Tumepokea ripoti kwamba boti ilikuwa imezama majira ya saa tano asubuhi na mara moja tukaanza operesheni ya kuwasaka watu watatu waliokuwa ndani, boti na magunia 15 yaliyokuwa yamezama baharini. Kwa sasa tumewaokoa watu wawili ilhali nahodha wa boti, mizigo na boti havijapatikana. Eneo hili lina mawimbi makali yanayotatiza msako,” akasema Bw Mote.

Shee-Mwanasha ni miongoni mwa vivuko vinavyotambulika kuwa hatari zaidi kwa mabaharia kwenye Bahari Hindi, Kaunti ya Lamu.

Vingine ni Mlango wa Tanu, Mlango wa Ali, Mlango wa Bomani, Mlango wa Shella, Manda-Bruno, kivuko cha Mkanda na Mlango wa Kipungani.

  • Tags

You can share this post!

Tatuwasco yapokea tuzo kwa usambazaji mzuri wa maji

Ufukuaji makaburi Shakahola waendelea, walioangamia ni 391

T L