• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
Tatuwasco yapokea tuzo kwa usambazaji mzuri wa maji

Tatuwasco yapokea tuzo kwa usambazaji mzuri wa maji

NA LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya kusambaza maji ya Tatuwasco imeteuliwa kama kampuni ya kibinafsi inayotoa huduma bora kwa wateja wake huu ukiwa mwaka wa pili mfululizo.

Bodi ya Kudhibiti Usambazaji wa Maji (WASREB) ilitangaza hayo mnamo Alhamisi wakati wa kupokeza Tatu City tuzo.

Kwa muda wa miaka kumi ambayo imepita kampuni hiyo ya Tatuwasco imewekeza mabilioni ya fedha kwa lengo la kusambaza maji safi kwa wateja wao.

Kampuni hiyo imekuwa ikihifadhi lita 15 milioni za maji kila mara kwa lengo la kusambaza kwenye shule tofauti, kwa wakazi wa Tatu City, na hata kwa kampuni zilizoko katika eneo hilo.

Kwa hivyo, kampuni hiyo imekuwa na jukumu kubwa la kusambaza maji kwa wingi kwa wakazi wote walio katika eneo hilo.

“Tuzo hii inathibitisha wazi kuwa kazi yetu ni safi na tayari tunasambaza maji kwa kipindi cha saa 24 mfululuzo kila siku bila kusita. Tunaheshimu mahitaji ya wateja wetu kila mara,” alifafanua meneja mkuu wa kampuni ya Tatuwasco Bi Caroline Cheptoo.

Alisema WASREB imekuwepo tangu mwaka wa 2016 chini ya sheria 721(a).

Tatuwasco ilisifiwa kwa usambazaji maji mzuri na uwajibikaji kwa kila mteja.

Alisema wateja wao wanapata maji safi huku wafanyakazi wao wakihudumia wateja kwa uwazi.

Meneja huyo alisema wateja wao wanahudumiwa kwa uwazi huku wakifanya marekebisho ya kila mara kwa mabomba yanayofuja.

Tatu City inajumuisha miradi mingi ya maendeleo ikiwemo miradi ya kibiashara ya Kenya Wine Agencies Ltd, Cooper K Brand, Davis & Shirtliff,  na majumba zaidi ya 3,000 yaliyojengwa katika eneo la ekari 5,000.

Majumba hayo yako wazi kununuliwa na wateja kutoka kote huku yakiwa na ukubwa tofauti.

Alisema eneo la Tatu City pia linajumuisha Kijani Ridge ambako pia kumejenga majumba mengi ya kukodisha.
  • Tags

You can share this post!

Maisha ya binadamu yana thamani kuliko maua, Sifuna...

Ajali: Wawili waokolewa mawimbi yakitatiza utafutaji wa...

T L