• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Amri watumishi wa umma wafichue mali zao

Amri watumishi wa umma wafichue mali zao

Na WALTER MENYA

WATUMISHI wa umma wamepewa hadi mwisho wa mwaka huu 2021 kutangaza utajiri wao kulingana na ilani iliyotolewa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Katika hatua inayonuiwa kubaini watakaodanganya na waliojipatia utajiri kwa njia isiyoeleweka tangu walipotangaza utajiri mara ya mwisho miaka miwili iliyopita, EACC inataka ofisi zitakazopokea fomu za kutangaza utajiri kuchanganua, kukagua na kuthibitisha na kuripoti wakipata rekodi si sahihi.

“Baada ya muda wa kutangaza utajiri kupita, kila afisi au tume italinganisha habari ilizopata kutoka kwa watu wengine na zilizotangazwa na afisa wa umma au kundi la maafisa wa umma,” alisema Afisa Mkuu wa EACC, Twalib Mbarak kwenye ilani aliyoandika Novemba 2.

Sehemu ya 26(1) ya sheria ya maadili ya watumishi wa umma inasema maafisa hao wanapaswa kutangaza utajiri wao kila baada ya miaka miwili.

Kila mmoja anafaa kutangaza mapato yake, mali na madeni na yale ya waume au wake wao na watoto walio na umri wa chini ya miaka 18.

Mara ya mwisho watumishi wa umma kutangaza mali yao ilikuwa 2019.

Baada ya shughuli hiyo, afisi zinazohusika zitawasilisha ripoti kwa EACC na kutoa orodha ya wale watakaokosa kutangaza utajiri wao, waliokataa kutoa ufafanunuzi wakiombwa kufanya hivyo na wale wanaoshukiwa kuwa na utajiri wasioweza kuthibitisha walivyoupata.

Kulingana na sheria ya maadili ya watumishi wa umma, ni kosa kukataa kutangaza utajiri au kuwasilisha tangazo lisilokamilika na kukataa kutoa ufafanuzi.

Wanaokiuka sheria hii wanaweza kutozwa faini ya Sh1 milioni, kufungwa jela mwaka mmoja au adhabu zote mbili.

You can share this post!

Yanayomsubiri Ruto akifurushwa Jubilee

Kinara wa KNUT amrukia Sossion kuhusu zogo

T L