• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Yanayomsubiri Ruto akifurushwa Jubilee

Yanayomsubiri Ruto akifurushwa Jubilee

Na CHARLES WASONGA

HISIA mseto zimeibuliwa kuhusu iwapo Naibu Rais Dkt William Ruto ataendelea kushikilia wadhifa huo endapo atapokonywa cheo cha Naibu Kiongozi wa Jubilee kutokana na uhusiano wake na chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Chama hicho tawala kimetangaza kuwa kitaandaa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wake (NDC) mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba ambapo mojawapo ya ajenda ni kumfurusha Dkt Ruto na wabunge washirika wake.

Kulingana na Katiba ya Jubilee, naibu kiongozi wake ndiye atashikilia wadhifa wa Naibu Rais chini ya serikali ya chama hicho.

Lakini kwa mujibu wa Katiba ya nchi, Rais Uhuru Kenyatta ambaye ndiye pia kiongozi wa Jubilee hawezi kumfuta kazi Dkt Ruto.

Hii ni kwa sababu kulingana na kipengele cha 136 cha Katiba Rais na Naibu wake huchaguliwa kwa tiketi moja.

Hata hivyo, wiki jana Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alisema kuwa chama cha Jubilee hakitaendelea kuwavumilia viongozi waasi ambao tayari wamekaidi sera na maongozi ya chama hicho na wanauza sera za chama kingine.

“Katiba ya chama chetu inasema wazi kwamba wale ambao wanaenda kinyume na sera zake watafurushwa. Hilo ni jambo muhimu zaidi kwa sababu kwa mujibu wa Katiba na sheria nyinginezo, mtu hawezi kuwa mwanachama wa vyama viwili kwa wakati mmoja. Kwa hivyo, hatua hii muhimu ya kuwafurusha wakaidi itaidhinishwa katika NDC ambayo ni asasi yenye usemi wa juu zaidi katika Jubilee,” Bw Tuju akawaambia wanahabari katika makao makuu ya chama hicho, Pangani, Nairobi.

TAREHE

Hata hivyo, Katibu huyo wa Jubilee hakutaja tarehe ya kongamano hilo akisema itawekwa kwa kuzingatia ratiba ya shughuli za Rais Kenyatta.

Akihutuhubu katika eneo la Kasikeu, Kaunti ya Makueni wiki jana Dkt Ruto kwa mara ya kwanza alitangaza hadharani kwamba atagura chama cha Jubilee na kujiunga rasmi na UDA.

“Tumekubaliana kwamba nitaondoka Jubilee ili nijikite sawa sawa ndani ya chama cha UDA ambacho ni chama cha kitaifa cha mahasla. Kauli mbiu yetu ni Kazi ni Kazi na niwasihi muungane nasi ili tuunde serikali inayoelewa changamoto zinazowasibu watu wa tabaka la chini kama vile mama mboga, waendesha bodaboda na wengine,” Dkt Ruto akaeleza.

Lakini wachanganuzi wa masuala ya kisheria wanasema kuwa kupinga kuondolewa kwa Dkt Ruto kutoka wadhifa wake wa Naibu Kiongozi wa Jubilee hakutaathiri cheo chake kama Naibu Rais wa Kenya.

Wakili James Mwamu anasema ingawa Katiba ya Jubilee inasema kuwa Naibu Kiongozi wake ndiye atashikilia wadhifa wa Naibu Rais, Katiba ya nchi inamkinga Dkt Ruto.

“Dkt Ruto ataendelea kushikilia cheo cha Naibu Rais hata akipokonywa wadhifa wake kama naibu kiongozi wa Jubilee. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa kipengele 136 cha Katiba, Rais na Naibu Rais huchaguliwa kwa tiketi moja na Rais hawezi kumfuta kazi naibu wake,” anaeleza.

“Vile vile, Dkt Ruto atasalia kuwa Naibu Rais hata kama atajiuzulu rasmi kutoka kwa chama cha Jubilee kwa kuwasilisha barua rasmi kwa afisi kuu ya chama hicho,” Bw Mwamu, ambaye zamani alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Afrika Mashariki (EALS), akaongeza.

Mbunge wa Makueni Daniel Maanzo, ambaye pia ni mwanasheria, anakubaliana na wazo la Bw Mwamu akishauri chama cha Jubilee kuelekeza juhudi zake katika mpango wa kukipa nguvu baada ya kudhoofishwa na maasi kutoka kwa Dkt Ruto na wandani wake.

“Kung’olewa kwa Dkt Ruto hakutakuwa na maana yoyote. Katiba ya Kenya inamlinda. Athari ambayo atapata ni ile ya kisiasa kwani atakuwa na wakati mgumu kujihusisha na mafanikio ya chama cha Jubilee huku akijitenga na mapungufu yake,” anaeleza mbunge huyo wa chama cha Wiper.

TAMBULIWA

Hata hivyo, Katibu wa Kundi la Wabunge wa Jubilee (PG) Aden Keynan anashikilia kuwa Dkt Ruto hatakuwa na haki ya kujigamba kwamba yeye ni Naibu Rais kwani hatakuwa anatambuliwa na chama tawala.

“Endapo wajumbe wa chama chetu watakubali mabadiliko ambayo Kamati ya Kitaifa Simamizi (NMC) imependekeza, bila shaka tutakatiza uhusiano wetu na Ruto pamoja na wabunge waasi wanaomuunga mkono. Wadhifa wa kiongozi wa chama utapanuliwa ili ushikiliwe na zaidi ya mtu mmoja,” akasema Mbunge huyo wa Eldas, bila kutoa ufafanuzi zaidi.

Bw Keynan ambaye aliongoza mkutano wa PG wa ushirikiano na Kiongozi wa Wengi Bungeni Amos Kimunya katika mkahawa wa Safari Park Alhamisi, alisema Jubilee itaanza ukurasa mpya baada ya kongamano la NDC litakalofanyika katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi.

“Tumeamua kuondoa uchafu ambao waasi hawa waliojiunga na UDA wameleta katika chama chetu. Tutawaondoa na kuanza upya. Mtu hawezi kuendelea kujiita Naibu Rais ilhali yeye ni mwanachama wa chama cha upinzani,” akaeleza huku akimrejelea Dkt Ruto.

Lakini mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anasema kwa kuendelea kushikilia wadhifa wa Naibu Rais Dkt Ruto ndiye atafaidi kwa sababu atakuwa akitumia mali ya umma kuendesha kampeni zake.

Anasema Jubilee inafahamu hali hii na ndio maana imemtumia Mbunge wa Ndaragua Jeremiah Kioni kudhamini mswada wa marekebisho ya Katiba ili Rais awe akiteua Naibu Rais.

Mswada huu una nafasi finyu ya kupita bungeni ikizingatiwa kuwa unahitaji kupitishwa na angalau wabunge 233.

“Itakuwa vigumu kwa idadi hii ya wabunge kufikiwa ikizingatiwa kuwa jumla ya wabunge 150 wanaegemea mrengo wa Dkt Ruto ambao tayari wameupinga mswada huu,” akaeleza Bw Andati.

  • Tags

You can share this post!

Mwamko mpya wanawake Pwani wakilenga ugavana

Amri watumishi wa umma wafichue mali zao

T L