• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Wazee wampongeza Uhuru kwa kusema ‘Ruto ni prezzo wangu’

Wazee wampongeza Uhuru kwa kusema ‘Ruto ni prezzo wangu’

NA MWANGI MUIRURI

WAZEE wa Mlima Kenya sasa wanawasihi viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua wakumbatie wito wa amani ambao Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alitoa Jumatatu.

Licha ya kugeuzwa vibonde na washirika wa Rais Ruto katika eneo la Mlima Kenya na Rift Valley katika siku za hivi karibuni, Bw Kenyatta alijitokeza akisema kwamba iwapo ataalikwa kikao na Rais Ruto, atakubali.

“Mimi siwezi nikajipeleka kukutana na Rais Ruto ikiwa hajanialika. Lakini akinialika, nitaenda kwa kuwa hata mimi yeye ni ‘prezzo wangu’,” akasema Bw Kenyatta katika mahojiano na vyombo vya habari akimaanisha anamtambua Ruto kuwa ni kiongozi wa nchi.

Sasa, mwenyekiti wa muungano wa wazee wa Mlima Bw Wachira Kiago amesema kwamba hiyo ni ishara tosha ya heshima na unyenyekevu kutoka kwa Bw Kenyatta.

“Amedumisha nembo yake na inagusa roho sana kumuona akitelekezwa kwa kiwango ambacho tumeshuhudia,” akasema Bw Kiago.

Bw Kiago alimtaka Bw Gachagua achukue jukumu la kuridhiana wanasiasa wa Mlima Kenya ambao wamekuwa wakimshambulia Bw Kenyatta kwa kiwango kikuu.

Baadhi ya washirika wa Rais Ruto wamekuwa wakimshutumu kwa ukali usio na kifani kwamba anafadhili maandamano dhidi ya serikali, anafufua kundi haramu la Mungiki na pia kuhujumu kukosa kumtambua Rais Ruto.

“Lakini Bw Kenyatta ameweka hisia zake wazi. Amekana madai hayo na kusisitiza kwamba isipokuwa tu kuwa rafiki wa kinara wa Azimio Bw Raila Odinga, hahusiki kamwe na matukio ya kisiasa yanayoendeshwa dhidi ya serikali,” akasema Mzee wa Murang’a Bw Kiarie Chombou.

Bw Chombou alisema kwamba “hatutaki huu mtafaruku ambao unatugawa kwa misingi ya uhasama wa kisiasa na sote tunafaa kuja pamoja kusaka maendeleo kwa watu wetu”.

Bw Chombou ambaye hivi majuzi alimkabidhi Bw Mwangi Njuguna hatamu za uenyekiti wa Kiama kia Ma alisema kwamba “ni aibu sisi kuonekana tukipigana wakati wengine wanaonekana kuungana”.

Bw Chombou alisema kwamba madai ya kumhusisha Bw Kenyatta na pia familia yake katika visa vya uvunjaji sheria na kisha kuona jina la Mama Ngina Kenyatta likiingizwa kwa siasa si haki.

Mwenyekiti wa muungano wa Gikuyu, Embu na Meru (Gema) Bw Lawi Imathiu alisema kwamba “umoja, amani na ustawi ndizo nguzo kuu za kijamii na ni vyema wote waungane na kuzika tofauti zao za kisiasa”.

  • Tags

You can share this post!

Azimio kuwasha mishumaa kesho Jumatano

Jinsi Tuntigi Gaming wanavyovutia vijana wanaotaka kucheza...

T L