• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Bei ya vyakula kuongezeka

Bei ya vyakula kuongezeka

NA BRIAN AMBANI

BEI ya bidhaa za vyakula huenda ikaongezeka zaidi kutokana na bei ghali ya vifaa na mafuta, kupungua kwa kiwango cha uzalishaji nchini ikiwemo gharama ya juu ya kuagizia bidhaa nchini.

Aidha, wakulima wameonya kuhusu kuongezeka kwa bei ya vyakula kama vile sukari, mkate, mchele, mafuta ya kupikia na bidhaa nyinginezo.

Utafiti uliofanywa na Benki Kuu ya Kenya (CBK) kuhusu Sekta ya Kilimo kati ya Mei 9 na 12 unaashiria kuwa bei ya bidhaa za vyakula itaendelea kuwa ghali mwezi huu na itakuwa kiini cha mfumko wa bei.

Utafiti huo ulitathmini mabadiliko katika bei za jumla na rejareja sokoni, matarajio ya kubadilika kwa bei na vifaa pamoja na masuala yanayoathiri sekta hiyo.

Kulingana na ripoti hiyo, msimu wa vua kubwa kati ya Machi na Mei ulikuwa chanzo cha bei kushuka kwa mazao ya muda mfupi kama vile mboga. Wakulima wa nyanya katika masoko ya Gilgil na Naivasha, kwa mfano, walisema mazao kutoka masoko makuu mjini Subukia yameongezeka pakubwa hivyo kusababisha bei kushuka.

Bei ya mahindi haikubadilika mnamo Mei.

Hata hivyo, bei ya aina fulani za mchele, maharage, viazi, sukari na ngano zilisalia juu kuashiria kuwa bado zinaandamwa na athari za kiangazi cha muda mrefu mwaka 2022, utafiti huo ulisema.

“Ingawa wakulima waliripoti kuongezeka kwa malisho kufuatia vua kubwa, bei za maziwa yaliyopakiwa na ambayo hayajapakiwa ziliongezeka pakubwa Mei kutokana na bei ghali za malisho na gharama za usafirishaji,” ilisema ripoti.

“Bei za mayai huenda zikapanda vilevile kwa sababu ufugaji wa kuku unategemea pakubwa lishe inayouzwa madukani. Bei za sukari zimesalia juu na huenda zikapanda hata zaidi kutokana na kupungua kwa miwa na gharama ya juu ya kuagizia mazao hayo nchini.”

Japo bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula kama vile mboga ilishuka Mei, bei ya bidhaa nyinginezo za vyakula kama vile sukari ilipanda ambapo pamoja na bei ghali za umeme gharama za usafiri, zilichangia mfumko wa bei kupanda kwa asilimia 0.1 au asilimia 1.26.

Kiwango cha mfumko wa bei kilifikia asilimia 8 mwezi uliopita kutoka asilimia 7.9 Aprili, kulingana na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS), huku familia zikilemewa na bei za bidhaa zinazozidi kupanda.

Gharama za makazi, maji, umeme, gesi na aina nyinginezo za kawi ikiwemo usafiri ziliathiriwa na kuongezeka kwa bei ya bidhaa za petroli huku bidhaa za petroli, dizeli na mafuta taa zikiuzwa kwa jumla ya Sh183.29, S h 1 6 9 . 1 0 n a Sh161.83 kwa kila lita mtawalia, kote nchini.

Bei ghali ya sukari iliathiri takwimu za bidhaa za vyakula na vinywaji visivyo pombe zilizopanda hadi asilimia 49.2 kila mwaka na asilimia 22.1 kila mwezi, huku kilo moja ya sukari ikiuzwa kwa jumla ya Sh194.29 mnamo Mei na kuanzia Sh159.10 Aprili.

  • Tags

You can share this post!

Mswada wa ushuru: Raila kutoa mwelekeo Alhamisi

Mary Moraa atarajiwa kuwa kivutio kwenye riadha za polisi

T L