• Nairobi
  • Last Updated June 1st, 2024 12:49 PM
Mswada wa ushuru: Raila kutoa mwelekeo Alhamisi

Mswada wa ushuru: Raila kutoa mwelekeo Alhamisi

Na LEONARD ONYANGO

KINARA wa Azimio Raila Odinga atatangaza Alhamisi mapambano dhidi ya Mswada wa Fedha wa 2023 unaopendekeza kuongezwa kwa ushuru wa bidhaa na huduma muhimu.

Bw Odinga jana alisema kuwa Upinzani watatoa taarifa ya kina kuelezea Wakenya kwa nini wanapinga mswada huo ambao umeibua mjadala mkali nchini.

Jumapili, Rais William Ruto alionya wabunge wa Kenya Kwanza watakaothubutu kupinga mswada huo kuwa wataadhibiwa.

Naye Bw Odinga jana aliwataka Wakenya kupambana na wabunge wao watakaounga mkono Mswada huo aliosema unalenga kukandamiza raia.

“Wabunge watakaounga mkono mswada huo watakuwa wasaliti kwa Wakenya,” akasema Bw Odinga.

Awali, kiongozi huyo wa Upinzani alikuwa ametoa makataa ya hadi Jumatatu kwa Rais Ruto kufanyia marekebisho Mswada huo la sivyo atangaze maandamano.

Mswada wa Fedha wa 2023 unapendekeza kupandishwa kwa ushuru wa bidhaa muhimu kama vile mafuta na kukata wafanyakazi asilimia 3 ya mishahara yao kwa ajili ya mradi wa nyumba.

Jana, Rais Ruto alijipata pabaya baada ya waandamanaji kukusanyika nje ya ukumbi wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Makazi (UN Habitat) mtaani Gigiri, Nairobi, wakipinga makato ya nyumba.

Kiongozi wa Nchi alisalia kimya alipowaona waandamanaji hao waliokuwa na mabango yaliyoandikwa: ‘Usilazimishie Wakenya ushuru wa nyumba’ na kisha kuondoka.

 

  • Tags

You can share this post!

Mahabusu wakodolea macho njaa serikali ikifilisika

Bei ya vyakula kuongezeka

T L