• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
Bodaboda za stima zaanza kuwaniwa watumizi wakisema hazihitaji fundi kila wakati

Bodaboda za stima zaanza kuwaniwa watumizi wakisema hazihitaji fundi kila wakati

NA FRIDAH OKACHI

IDADI ya Wakenya ambao wamekumbatia matumizi ya pikipiki za umeme imeanza kuimarika kwa miezi michache iliyopita.

Wauzaji wa pikipiki hapa jijini Nairobi, wanasema wamekuwa wakishuhudia ongezeko hilo kila uchao.

Jimmy Tume ambaye ni mmiliki wa kampuni ya E-Worker Mobility na muuzaji wa pikipiki za umeme jijini Nairobi, anasema punde tu baada ya kuongezeka kwa bei ya mafuta, kumeshuhudiwa ongezeko la Wakenya wanaokimbilia pikipiki za umeme.

Kampuni ya E-Worker Mobility inauza baiskeli za umeme na pikipiki za umeme, tofauti ikiwa ni kuwa baiskeli wanawapa vijana kufanyia kazi na kurejesha ila kwa pikipiki wanauza kati ya Sh200,000 – Sh250,000.

“Pikipiki hizi ni za kudumu haswa wakati huu bei ya mafuta imepanda. Pikipiki za kitambo utanunua na Sh160, 000. Kununua mafuta utagharamika kwa Sh10, 000 –Sh15, 000 kila mwezi,” asema Tume.

Kulingana na Tume utumiaji wa pikipiki ya umeme, haupotezi wakati kupeleka kwenye kituo cha kutengenezwa kila wakati.

Tume anaelezea kuwa kuna pikipiki za umeme mara mbili ambazo anauza, aina ya kwanza ikiwa ni ile unatumia tokeni za nyumbani kuongeza nguvu za umeme.

Aina ya pili ikiwa ni ile ambayo utahitajika kwenda kwenye kituo cha kuongeza umeme kwenye betri.

Kuhusu usafiri, asema pikipiki ya umeme ina manufaa yake, kwa wale wanatumia tokeni wakitumia Sh50 kwa siku. Kwa wale wanaotumia kituo kuongeza umeme kwenye betri ikiwa ni Sh100 kwa siku.

Kwa mujibu wa wahudumu wa bodaboda, licha ya kuwepo changamoto kama vile vituo vya kuchaji au kuongeza umeme, ni nafuu ikizingatiwa kwa sasa bei ya mafuta imepanda zaidi.

Derick Wanjohi, mhudumu wa bodaboda jiji Nairobi, anatumia pikipiki ya umeme. Anasema inamfurahisha kutokana na kuwa haina kelele na huleta starehe ikilinganishwa na ile ya awali aliyokuwa akitumia.

Hata hivyo, licha ya pikipiki hiyo ya stima kuwa yenye manufaa kwa mhudumu wa chini, inauzwa kwa bei ghali.

Pikipiki hiyo ya stima inaenda mwendo mfupi ikilinganishwa na pikipiki za kawaida kutokana na utumiaji betri.

Wanjohi anasema kuwa kinachomtatiza ni kuwa wakati betri yake inaisha nguvu, hulazimika kubadilisha na kupeleka iliyoisha umeme kwenye kituo cha kuchaji. Betri hiyo ikichukua muda wa saa nne ndiposa kutumika tena.

Gordien Nijimbere, mhudumu wa bodaboda katika mtaa wa Kawangware, anayo matamanio ya kuwa na pikipiki ya stima.

Nijimbere anasema kuwa amemshuhudia mwezake ambaye ana pikipiki ya stima ambayo haina gharama nyingi ikiinganishwa na anayotumia.

“Nikimaliza mkopo wa pikipiki hii lazima nitanunue hii ya stima ndio niweke hizi Sh500 za carburator,” akielezea Nijimbere.

Nijimbere hutumia Sh200 kubadilisha kichujio cha mafuta ‘oil filter’ mara mbili kwa mwezi, Sh1,000 kubadilisha mafuta mara mbili kwa mwaka, jambo ambalo anahisi kuwa mzigo kwake ilhali anaweza wekeza pesa hizo kwa mahitaji mengine ya pesa.

Aidha, suala la bei ya pikipiki zenyewe linasalia kizingiti kikubwa kwa baadhi ya Wakenya ambao wanasema mapato yao ni madogo.

Mwenyekiti wa wahudumu wa bodaboda, kaunti ndogo ya Dagoretti, George Kamaru, akisema kuwa kufikia sasa eneo lake kuna vijana 7 wanaotumia pikipiki za umeme.

Rais William Ruto akizungumza mapema mwezi huu katika kongamano la mabadiliko ya tabianchi, alisisitiza haja ya kumaliza kabisa matumizi ya magari na pikipiki za petroli, kutokana na uchafuzi wa mazingira.

  • Tags

You can share this post!

Mjane, 64, alivyokita katika ushonaji kofia kukabili upweke...

Mshukiwa wa ulaghai wa Sim Card ajipeleka Safaricom na...

T L