• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Mjane, 64, alivyokita katika ushonaji kofia kukabili upweke wa kufiwa na mumewe mapema

Mjane, 64, alivyokita katika ushonaji kofia kukabili upweke wa kufiwa na mumewe mapema

NA KALUME KAZUNGU

NI taaluma aliyoipenda tangu akiwa binti mchanga wa umri wa miaka 20 pekee.

Na sasa akiwa ametinga umri wa miaka 64, Bi Khadija Hakofa Dawa katu hafikirii kuiacha tasnia hiyo ambayo ameiweka mahali pema katika chemba cha moyo wake.

Akidumu katika ushonaji wa kofia hizo za vito kwa miaka 44 sasa, Bi Hakofa anasema kilichomsukuma zaidi kujikita kwenye kazi hiyo ni kifo cha mumewe kilichotokea karibu miaka 30 iliyopita.

Kwa kawaida, tamaduni za baadhi ya jamii za Afrika hupendekeza wanawake wanaofiwa na waume wao na kuachwa wajane wakiwa na umri mchanga kurithiwa na ndugu ya marehemu mumewe au mtu mwingine wa nasaba hiyo, japo kwa hiari na wala si kwa kulazimishwa.

Kwa Bi Hakofa, aidha, yeye anasema aliamua kulitupa penzi lake katika kazi hiyo ya kushona.

Kwa wanaomjua Bi Hakofa wanasema kila kuchao, iwe ni asubuhi na mapema, mchana au jioni, utampata Bi Hakofa akiwa amekaa kitako mkekaki kwa umakinifu mkuu, akiwa amepataka kitambaa, nyuzi na shindano maalum akiendeleza utengenezaji wa kofia za vito.

Kofia ya vito. PICHA | KALUME KAZUNGU

Ajuza huyo, ambaye ni mama wa watoto watano na wajuukuu kadhaa, ni mkazi wa mtaa wa Kandahar kisiwani Lamu.

Katika mahojiano na Taifa Leo nyumbani kwake, Bi Hakofa alisema angalau ushonaji wa kofia umedhihirisha wazi kuwa mfariji wa kipekee kwake.

Anaeleza kuwa punde anapoanza kushona, fikra ya machungu ya kuondokewa na mumewe husahaulika au kufutika kabisa, japo kwa muda tu.

Anasema kila anapoanza kazi ya kushona, yeye huzamisha mawazo yake yote kwenye shughuli hiyo, hivyo kumbukumbu ambazo zingeiteka na kuitawala akili yake kumhusu marehemu mumewe hukosa nafasi ya kupenya.

“Mume wangu alinioa nikiwa na miaka 16 pekee. Sikusoma. Ndiye aliyenifunza huu ujuzi wa kushona kofia na nikaukumbatia vyema. Alikuwa kila akienda kazini kusaka tonge, mimi pia ninabaki nyumbani kutunza boma na kushona. Ni kazi ambayo iliniwezesha kujipatia kipato na kumsaidia mume wangu kukimu mahitaji ya familia yetu hadi alipotangulia mbele ya haki. Mume wangu alipofariki aliniacha na watoto watano, ambao ni mabinti watatu na vijana wa kiume wawili,” akasema Bi Hakofa.

Anasema ni kupitia ushonaji wa kofia za vito ambapo umemwezesha kuikimu familia yake, hasa kwa chakula, mavazi na hata elimu.

“Punde mume wangu alipofariki, nilipata shinikizo si haba kutoka kwa jamii kwamba niolewe. Nikadinda. Nikaona haina haja kukaribisha mume mwingine nafsini mwangu. Katika harakati za kujifariji, kujiliwaza na kusahau kifo cha mume wangu, nikaamua kujitosa mzimamzima kwenye huu ushonaji wa kofia badala ya kuolewa. Mbali na kwamba hii ni kazi niliyofunzwa na marehemu mume wangu, nafsi yangu yenyewe imeipenda kwani imenipatia mtaji wa kuendeleza familia yangu niliyoachiwa na kipenzi changu cha moyo,” akasema Bi Hakofa.

Ujuzi huo amefaulu kuupitisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwani tayari mabinti wake wawili wawili ni magwiji kwenye ulingo wa kushona kofia za vito.

Bi Salma Mohamed ambaye ni bintiye Bi Khadija Hakofa Dawa. Yeye alipokezwa ujuzi wa kushona kofia za vito na mamake ambaye ni Bi Hakofa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Isitoshe, baadhi ya wajukuu wake pia wamevutiwa na maarifa hayo ya kushona kofia za vito na tayari wako mbioni kujifunza.

“Mabinti wangu walikuwa kila wakitoka shuleni hujumuika na mimi katika kushona kofia za vito. Leo hii kuna wawili ambao wameolewa na ni wajuzi sana wa kutengeneza hizi kofia na wanasaidia mabwana zao kujikimu maishani. Kuna wajukuu wangu ambao pia hivi karibuni watakuwa wajuzi kwani wameibukia sana kupenda kushona,” akasema Bi Hakofa.

Anatoa wosia kwa wajane kwamba wanapaswa kufanya uamuzi wao binafsi kuhusu jinsi wanavyotaka kuishi.

Bi Hakofa anashikilia kuwa wajane hawafai kulazimishwa kurithiwa na jamaa za marehemu.

Anasisitiza kuwa la muhimu na kimsingi ni kuwa mwisho wa ndoa ni kifo na wajane wana uhuru wa kuamua wanavyotaka kuishi baada ya waume zao kuaga dunia.

“Haina haja wewe kama mjane uhangaishwe bure. Watu wafahamu kwamba kurithi wajane hakuna msingi wa kisheria. Unaweza kuamua kuolewa tena au ubaki vivyo hivyo kama mimi. Ifahamike wazi kuwa ndoa ni muungano wa hiari kati ya mwanamume na mwanamke. Kulazimisha mjane kuolewa, iwe na ndugu au jamaa wa familia au ukoo ni kinyume cha sheria,” akasema Bi Hakofa.

Baadhi ya wakazi waliohojiwa na Taifa Leo walisema wao mara nyingi hupendelea kutengenezewa kofia zao na Bi Hakofa.

Walimsifu mjane huyo kwa ujuzi alio nao na walioutaja kuwa wa aina yake.

Bw Khamis Athman anasema badala ya kuenda dukani kununua kofia za vito ambazo mara nyingi zinakosa uhalisia wa Lamu, yeye humlipa Bi Hakofa mapema ili kumuundia kofia kindakindaki ya vito ya Lamu.

“Siku hizi hizi kofia zetu za vito za Lamu zimeanza kuigwa hata na Wachina. Utapata kofia ya Lamu ikiuzwa dukani kwa bei rahisi lakini ukiifunua utaona kibandiko kwamba imeundwa China. Mwonekano wake huwa sawa, lakini ukweli ni kwamba si asili ya Lamu. Wachina wanatengeneza kofia kwa mashini ilhali wenyeji wa Lamu huzitengeneza kofia hizo kwa mkono, hivyo kuwa za kipekee. Na hiyo ndiyo sababu hufaharika na kuienzi kazi ya Bi Hakofa,” akasema Bw Athman.

Kofia ni vazi muhimu linalovaliwa kichwani.

Katika kaunti ya Lamu, kofia hii ya vito au vitho ni maarufu sana kwani huhusishwa sana na utamaduni wa Waswahili wanaoishi hasa kwenye mwambao wa Pwani.

Gharama ya kutengeneza kofia hizi hadi kukamilika kwake huwa ni kati ya Sh8,000, ambayo ndiyo bei ya chini kabisa, hadi Sh45,000 kulingana na mtindo au umaalum ambao mteja anataka.

Muda unaotumiwa kushona na kukamilisha kofia za vito kwa mkono ni kati ya miezi miwili au mitatu.

Wanaovaa kofia halisi za vito na kuzitunza vyema hudumu nazo kwa kati ya miaka 10, 15 au hata 20.

  • Tags

You can share this post!

Aliyetaka kula tunda kwa nguvu ameomba msamaha akitaka...

Bodaboda za stima zaanza kuwaniwa watumizi wakisema...

T L