• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Bwanyenye wa Amerika akashifu serikali ya Ruto kwa kutenga Jumatatu kuwa Sikukuu ya upanzi miti

Bwanyenye wa Amerika akashifu serikali ya Ruto kwa kutenga Jumatatu kuwa Sikukuu ya upanzi miti

NA LABAAN SHABAAN

MTAALAMU wa Teknolojia ya Fedha (Fintech) ambaye ni mwajiri nchini Kenya, Jason Marshall, amekashifu serikali kwa kutangaza Jumatatu, Novemba 13, 2023 kuwa Sikukuu.

Serikali ilishangaza Wakenya kwa kutangaza kuwa leo, Jumatatu itakuwa Sikukuu kwa minajili ya upanzi wa miti nchini.

“Siku hii, wananchi wote wanatarajiwa kupanda miti kuonyesha uzalendo kwa juhudi za kitaifa za kuokoa nchi dhidi ya athari mbaya ya mabadiliko ya tabianchi,” alitangaza Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki kupitia Gazeti Rasmi la Serikali Novemba 6, 2023.

Tangazo hili lilimkera Bw Jason Marshall, ambaye ni mwajiri kutoka Amerika akishangaa ni kwa nini wafanyakazi wake washerehekee upandaji miti, badala ya kufanya kazi.

Afisa kutoka Shirika la Kulinda Misitu Nchini (KFS) akipanda mche wa mti katika shamba la Chuo Kikuu cha Nairobi, Bewa la Upper Kabete, Kiambu hapo awali. PICHA|SAMMY WAWERU

“Kuna Sikukuu nyingi sana Kenya. Wafanyakazi wetu wa Kenya hawatakuwa kazini Jumatatu ili waadhimishe siku ya kupanda miti. Hii ni nini sasa?” Bw Marshall alisikitika katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X (awali Twitter).

Mwajiri huyu amelinganisha taifa la Kenya na America (US), akisema nchi yake ina Sikukuu chache.

Kulingana na Bw Marshall, Kenya husherehekea Sikukuu ambazo hazina maana.

Mkurugenzi Mkuu Platinum Credit Ltd, Oscar Murigi akinyunyizia maji mche wa mti katika shamba Chuo Kikuu cha Nairobi, Bewa la Upper Kabete, Kiambu hapo awali. PICHA|SAMMY WAWERU

“Kule Amerika, Sikukuu ni za serikali na wafanyakazi wa benki tu,” alisema.

“Wanabenki na wafanyakazi wa serikali huwa na Sikukuu 11. Wafanyakazi wa sekta ya kibinafsi huwa na siku ya mapumziko 7 ama 8 Amerika,” aliongeza.

Kulingana na bwanyenye Marshall, kampuni yake itagharamika kulipa wafanyakazi wake licha ya wao kuadhimisha Sikukuu ambayo anasema walipewa bure.

Mche wa mti uliopandwa katika shamba la Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), Bewa la Upper Kabete, Kiambu. PICHA|SAMMY WAWERU

Siku hii, serikali inalenga kupanda miche 100 milioni kote nchini.

Wakenya wanaoshiriki upandaji miti wanatakiwa kupokea miche kutoka kwa afisi za chifu zilizo karibu nao bila malipo.

Mwaka uliopita, 2022, Rais William Ruto alizindua kampeni ya upanzi wa miti bilioni 15 kufikia 2032.

Mwananchi akipanda mti katika shamba la Chuo Kikuu cha Nairobi, Bewa la Upper Kabete, Kiambu. PICHA|SAMMY WAWERU
  • Tags

You can share this post!

Gari la nishati ya jua ambalo ukilikumbatia litakupunguzia...

Shughuli ya upanzi miti yaanza kote nchini

T L