• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Chanjo ya kuzuia corona yaharibika

Chanjo ya kuzuia corona yaharibika

Na ANGELA OKETCH

CHANJO za kuzuia corona zinaharibika katika baadhi ya sehemu nchini kwa sababu idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kuchanjwa, Taifa Leo imebaini.

Huku serikali ikiendesha kampeni inayolenga kuhakikisha kuwa jumla ya watu 10 milioni wamepata chanjo ifikapo Desemba 25, dozi zaidi zinapelekwa katika kaunti. Lakini imeripotiwa kuwa baadhi ya hospitali katika kaunti zilizoko maeneo kame nchini zimeripotiwa kutupa chanjo baada ya mikebe yake kufunguliwa kwa saa sita na kukosa watu wa kuchanjwa.

Hali hii imechangia Wizara ya Afya kutoa maelezo kwamba chanjo ya Johnson & Johnson zilizopelekwa katika maeneo kame bado inaweza kuhifadhiwa katika jokovu hata baada ya kufunguliwa. “Tunachukuwa chanjo tulizopeleka katika kaunti kame kutokana na sababu kadha.

Mojawapo ni changamoto ya uhifadhi kwa sababu ni idadi ndogo ya watu wanajitokeza kuchanjwa. Sababu nyingine ni kwamba kuna changamoto za uchukuzi katika maeneo hayo,” akaeleza Dkt Willis Akhwale, mwenyekiti wa jopokazi inayosimamia shughuli ya utoaji chanjo ya kuzuia Covid-19.

Dkt Akhwale aliamuru hospitali mbalimbali katika maeneo kame nchini kutoharibu dozi hizo mradi zimewekwa katika jokovu.“Hata baada ya kufunguliwa, ikiwekwa katika jokovu, chanjo zinaweza kudumu kwa hadi miaka miwili. Kwa hivyo, chanjo aina ya Johnson & Johnson haifai kuharibiwa kwa baada ya kutotumika,” akaeleza.

Data kutoka Wizara ya Afya inaonyesha kwamba kufikia Jumatatu, kaunti 10 ambazo ziliandikisha idadi ndogo ya wanaojitokeza kupata chanja zilijumuisha Mandera, Turkana, Pokot Magharibi, Wajir, Marsabit na Tana River.

You can share this post!

Wahadhiri, wahudumu wa vyuo vikuu vya umma watishia kugoma

Kaunti kusaidia manesi wanaotaka kwenda ulaya

T L