• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
El Nino: Uhaba wa mafuta Lamu kina mama wajawazito wakijifungua maeneo yaliyofurika   

El Nino: Uhaba wa mafuta Lamu kina mama wajawazito wakijifungua maeneo yaliyofurika  

NA KEVIN MUTAI

HUENDA shughuli za usafiri na uchukuzi katika Kaunti ya Lamu zikatatizika baada ya mafuriko yanayoshuhudiwa kuchangia uhaba wa mafuta.

Boti ambayo ndiyo mojawapo ya njia kuu za usafiri, imetatizika kutokana na mvua ya El Nino inayoendelea.

Hali hiyo imechangiwa na maji ya mafuriko ambayo yameharibu sehemu mbili za barabara kutoka Mokowe kuelekea Minjila, ikiathiri uchukuzi ndani na nje ya kaunti ya Lamu.

Mto Tana kuvunja kingo zake, kumewalazimisha wakazi kutegemea maboti kusafiri kutoka sehemu zilizoathirika huku ikiwagharimu angalau Sh500.

Hali hiyo imezidi kuwa mbaya zaidi, shirika la Msalaba Mwekundu, likieleza kuwa kambi nne za kuwasitiri waliopoteza makazi yao zilikuwa zimefurika na kusababisha watu kuhama.

Afisa wa walinzi wa fukwe na uokoaji Bi Susan Mtakai, anaeleza wasiwasi wa akina mama kujifungua kabla ya muda na ukosefu wa huduma za ujawazito ni suala kuu.

“Tunawaokoa watu ila akina mama na watoto ndio wameathirika sana. Tumekuwa na visa vya akina mama kujifungua katika maeneo yaliyofurika na ni jambo la kutia wasiwasi. Tunaomba msaada kutoka kwa wasamaria wema,” akasema Bi Mtakai.

Haya yanajiri, mshirikishi wa ukanda wa Pwani Bi Rhoda Onyancha akihoji kuwa serikali ilikuwa ikiwahamisha watu kutoka eneo hilo kwa ushirikiano na maafisa wa ulinzi na kaunti ya Lamu.

“Serikali imekuwa ikisambaza chakula na bidhaa nyingine muhimu kwa kutumia ndege. Vijiji vya Ozi na Kipini vimezingirwa na maji na haviwezi kufikiwa kwa njia ya barabara au kwa boti,” akasema Bi Onyancha.

Kulingana naye, “Viwango vya mafuta vimeenda chini katika kaunti ya Lamu na tunawazia kutumia meli za kijeshi, kusafirisha bidhaa adimu hadi kule ila tunatathmini hali.”

Kulingana na mshirikishi wa shirika la Msalaba Mwekundu ukanda wa Pwani, Bw Hassan Musa, watu 2,119 wameathirika kaunti ya Lamu, 500 kati yao wakipoteza makazi yao.

“Tumejenga kambi za kuwahifadhi na kuwapa chakula na bidhaa nyinginezo kama vile blanketi na neti za kuzuia mbu. Tumegundua kuna watoto wengi na akina mama wanaonyonyesha ambao wamekwama na wanahitaji msaada,” akasema Bw Musa.

Familia zilizoathirika zimeitaka serikali kuingilia kati na kuwasaidia kuhamia sehemu salama na kujenga makazi ya muda.

Aidha, ripoti zimeeleza kuwa wanaougua magonjwa mbalimbali hawawezi kufikia hospitali za daraja ya tano, na kulazimika kupata matibabu kwa hospitali zilizopo Lamu.

“Kuna wale ambao hawawezi kumudu gharama ya kusafiri kwa ndege kupata matibabu zaidi. Serikali itabidi iangalie hali hiyo na kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji huduma za rufaa,” akasema Bw Musa.

Huduma za uchukuzi wa umma nazo zimekuwa kizungumkuti, kusafiri ikigharimu zaidi ya Sh 2, 000 ikilinganishwa na Sh1, 500 ya kawaida.

Katika kaunti jirani ya Tana River, kambi 88 zimejengwa ili kuwashughulikia watu 11,167 ambao wamepoteza makazi yao kwa mafuriko hayo.

Kufikia sasa, shughuli za kuokoa walio katika vijiji vilivyozingirwa na maji zinaendelea.

 

  • Tags

You can share this post!

Vijana wahimizwa kutumia kozi zao kujiajiri

Avokado ni dhahabu shambani mwake  

T L