• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Avokado ni dhahabu shambani mwake  

Avokado ni dhahabu shambani mwake  

NA SAMMY WAWERU

KIJIJI cha Nyamesocho katika Kaunti ya Kisii ni chenye shughuli chungu nzima, kuanzia kilimo, ufugaji na biashara.

Kwenye shamba la Shem Oseko, mkaazi, amelipamba kwa mseto wa matunda na mimea.

Kilimo cha avokado, hata hivyo kina mvuto zaidi Oseko akikiri kimemsaidia kubadilisha maisha yake.

Alikiingilia zaidi ya miaka kumi iliyopita, baada ya kile anachotaja kama kuangushwa na kahawa.

“Soko la kahawa lilipoyumba, sikuwa na budi ila kutafuta njia mbadala kujiendeleza kimaisha,” anasema.

Anasema uamuzi na chaguo lake 2012 kuingilia ukuzaji maparachichi (avokado), kamwe hajutii.

Akiwa na jumla ya miparachichi 64, Oseko anadokeza kwamba alianza kwa kuvuna kilo 100 hadi 200 kila msimu.

Mkulima Shem Oseko aliingilia ukuzaji wa avokado baada ya soko la kahawa kumtesa. Amesalia na mikahawa michache. PICHA|SAMMY WAWERU

Kwa sasa, anachezea kati ya tani moja hadi tani moja na nusu, sawa na zaidi ya kilo 1, 000.

“Nilipoingilia ukuzaji avokado, mabroka walikuwa wanatuhangaisha ajabu; kilo moja walikuwa wananunua kati ya Sh50 – 60,” anadokeza.

Bei hiyo, ni hasara ikizingatiwa kazi ambayo mkulima amefanyia shamba lake ili kupata mazao.

Soko, hata hivyo, limeboreka na sasa ana kila sababu ya kutabasamu, shukran kwa Kenya Crops and Dairy Market Systems (KCDMS) kupitia mpango wa United States Agency for International Development (USAID) unaolenga kupiga jeki wakulima kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.

Hata ingawa KCDMS imekunja jamvi mikakati yake, Oseko anasema ilisaidia kumuunganisha na soko lenye ushindani mkuu.

“Nilianza kunufaika kupitia KCDMS 2019, na ni kupitia jukwaa la shirika hilo lililokuwa likifadhiliwa na USAID niliunganishwa na kampuni ya Biofarms,” akaambia Akilimali wakati wa mahojiano shambani mwake Kisii.

Biofarms Limited, kampuni yenye makao yake Kenya na ambayo kando na kuuza mazao nje ya nchi, hukuza mseto wa matunda, kuyapakia na kuyatafutia soko.

Matunda hayo yanajumuisha maparachichi, maembe, mananasi, na karakara (passion fruits).

Kampuni hiyo huuza mazao nchi za Bara Uropa (EU), Asia – China, Hong Kong, Malaysia, Singapore, na Milki ya Kiarabu ya Mashariki.

Mkulima Shem Oseko akikagua avokado shambani mwake. PICHA|SAMMY WAWERU

Masoko mengine ni Afrika Kusini, Morocco na Misri, Oseko akifichua kwamba bei ya Biofarms kilo moja ya avokado haipungui Sh100.

“Kwa mfano, msimu uliopita kilo moja ilinunuliwa Sh120.”

Licha ya kuwa safari yake katika kilimo cha maparachichi haijakuwa rahisi, akilalamikia gharama ya juu ya uzalishaji, Oseko anasema Biofarms imemnoa kuendeleza zaraa kwa utaalamu.

Oseko anasema, siri kupata mazao ya kuridhisha ni kutunza miparachichi.

Mosi, anasema Kisii eneo analoendeleza kilimo chake kando na kuwa na mvua ya kutosha, huhakikisha kila baada ya mavuno anaanza kuweka mbolea kwenye mashina ya miti.

“Sanasana mbolea ya kuku ndiyo bora zaidi. Huiweka kwa wingi,” asema.

Inapokosekana, hutumia samadi ya ng’ombe iliyoiva sambamba.

Hali kadhalika, hunawirisha mazao kwa kutumia fatalaiza hasa mvua inapoanza kunyesha.

“Kuanzia 2019, baada ya Biofarms kuletwa kwetu na KCDMS na kutufunza mbinu kuboresha mazao, kiwango kiliongezeka hadi baina ya kilo 1, 000 na 1, 500, kutoka kilo 200,” anaelezea.

Shem Oseko anaridhia kilimo cha maparachichi. PICHA|SAMMY WAWERU

Msimu uliopita, kwa mfano alivuna kilo 1, 500.

Baadhi ya miparachichi, anasema huzalisha wastani wa kilo 100 kwa msimu.

Biofarms, ina programu za mafunzo kwa wakulima wanachama jinsi ya kuzalisha matunda kitaalamu.

Kampuni hiyo hutoa mafunzo kwa wakulima wanachama wake jinsi ya kukuza avokado kwa ustadi.

Mafanikio katika kilimo chochote kile yanategemea uwepo wa maji, Daniel Mwenda, mtaalamu, akisisitiza ukuzaji matunda unataka chanzo cha raslimali hiyo ya kutosha.

“Kando na maji, mbolea na fatalaiza kunawirisha mazao, mkulima ahakikishe anadumisha usafi wa shamba,” Mwenda anahimiza.

Usafi wa shamba, ni kuhakikisha kuwa makwekwe yanadhibitiwa kupitia palizi.

Mtaalamu Mwenda ni mwasisi wa shirika la kibinafsi la Mavuno Agroforestry, linalotoa huduma za ukuzaji miti, ikiwemo ya matunda.

Shem Oseko anasema anajaribu kadri awezavyo kuhakikisha anaendeleza kilimoasilia, kwa kutumia mbolea ya mifugo kuzalisha avokado.

Alipoulizwa ikiwa anajivumia ukuzaji wa matunda hayo ya thamani alijibu, “Bila shaka, na ndio maana ninakiri kwamba hii ni ofisi yangu. Kilimo cha maparachichi kimeniandika kazi, wanangu ninawasomesha kupitia mapato ya matunda haya.”

Aidha, hukuza avokado aina ya Golden Hass.

Anahudumu chini ya kundi la wakulima 50, anaosema wako kwenye mikakati kulisajisili ili wanufaike kupitia mashauri ya Horticultural Crops Directorate (HCD) na Agriculture and Food Authority (AFA).

  • Tags

You can share this post!

El Nino: Uhaba wa mafuta Lamu kina mama wajawazito...

Kindiki atakiwa kutuliza uhalifu Pokot Magharibi

T L