• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Gachagua aapa kutounga handisheki ya Ruto na Odinga

Gachagua aapa kutounga handisheki ya Ruto na Odinga

SIMON CIURI NA WANGU KANURI

NAIBU wa Rais Rigathi Gachagua ameapa kutoshirikiana katika handisheki kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Akizungumza katika kanisa la AIPCA Limuru, kaunti ya Kiambu, Bw Gachagua alisema kuwa iwapo handisheki itakuwepo yeye atakaa mbali.

Matamshi yake yamejiri wakati vuta nikuvute kati ya viongozi wanaounga mkono Rais Ruto na Bw Odinga kuhusiana na handisheki, inaonekana kutikisa mawimbi ya kisiasa.

“Ikiwa kutakuwepo na handisheki, mimi sitakuwepo. Mnajua kile hutokea kila wakati wa handisheki na Bw Odinga. Mliona kilichomfanyikia aliposhirikiana na aliyekuwa kiongozi mmoja wetu aliyepewa heshima. Mliona jinsi mambo yalivyoanza kuharibika,” akasema Naibu Rais

Kauli ya Gachagua iliungwa mkono na gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi ambaye alisema kuwa ajenda ya handisheki haiwezi ikapigiwa debe na naibu wa rais, Gachagua.

Wamatangi aliyekuwa akimmiminia sifa Bw Gachagua alisema kuwa kiongozi huyo husema yaliyo moyoni pasi uoga.

“Niliona meseji ya watu wa Bw Odinga ikisema kuwa hawezi akakubali handisheki na Bw Gachagua. Msiwe na wasiwasi. Tunajua ni nini kilimfanya afikirie tena. Hakuna mwanasiasa wanayeogopa kama wewe.”

Akaongeza, “Hii ni kwa sababy unapoanza kuongea, mambo huchukua mkondo tofauti. Kwa hivyo msitishiwe. Hakuna nusu mkate.”

Kabla Rais Ruto kuchukua usukani, Bw Kenyatta alishiriki kwa handisheki na Bw Odinga.

Wawili hao hawakuwa wakionana jicho kwa jicho walipokuwa waking’ang’ania kiti cha urais mwaka wa 2017 na ‘uadui’ wao kisiasa ukaenea zaidi Bw Kenyatta alipotangazwa kama rais katika uchaguzi wa kurudia wa Oktoba 2017.

Hata hivyo, baada ya handisheki, wawili hawa wakawa marafiki wa dhati huku Rais Ruto ambaye wakati huo alikuwa naibu rais akiwa pembeni.

Uhusiano wa Kenyatta na Ruto ukasambaratika huku akiapa kutoshiriki katika salamu za maridhiano atakaposhinda uchaguzi wa 2022.

 

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa wa Sagini kung’olewa macho wana kesi ya...

Wito Kenya Power itumie tariff maalum kwa kampuni za maji

T L