• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Maseneta wakosa kuzima nyota ya Mwangaza

Maseneta wakosa kuzima nyota ya Mwangaza

NA MWANDISHI WETU

GAVANA wa Meru Kawira Mwangaza ambaye amekuwa na kibarua kigumu kujitetea mbele ya maseneta ana kila sababu ya kutabasamu baada ya kesi dhidi yake kuamuliwa saa sita usiku wa kuamkia Alhamisi ambapo maseneta walipiga kura, Bunge la Seneti likishindwa kumng’oa ofisini.

Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Jumanne iliamuliwa baada ya maseneta kusikiliza ushahidi wa madiwani na kumpa nafasi Gavana Mwangaza kujitetea. 

Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi alifafanua kabla ya shughuli ya upigaji kura, akisema maseneta wangepiga kura kwa kila mojawapo ya mashtata dhidi ya Gavana Mwangaza. Maseneta walipiga kura mara saba.

Shtaka la kwanza lilikuwa ni ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali za kaunti. Maseneta 19 walipiga kura ya kukubaliana na madiwani huku maseneta 28 wakipiga kura ya ‘La’.

Shtaka la pili lilikuwa upendeleo wa jamaa na ukiukaji mwingine wa maadili. Maseneta watano waliunga mkono ang’olewe huku 42 wakipinga.

Katika shtaka la tatu la kuwadhalilisha viongozi wengine kura ilipigwa ambapo matokeo yalikuwa kwamba watatu walikubaliana na madiwani wa Meru huku 44 wakipinga.

Kwenye shtaka la nne, Gavana Mwangaza alimulikwa na madiwani kwa kufanya uteuzi unaokiuka mchakato unaohitajika ambapo katika upigaji kura, maseneta 20 wamekubaliana na madai hayo huku 27 wakipinga.

Nalo shtaka la tano likihusu kuidharau mahakama ambapo maseneta watatu wamekubaliana na madiwani lakini wakalemewa na 44 waliopinga.

Aidha kiongozi huyo wa Kaunti ya Meru alikabiliwa na shtaka la sita la kuipa barabara jina la mume wake Bw Murega Baichu. Maseneta wanne wamepiga kura ya ‘Ndiyo’ ambapo tena walilemewa na 43 waliopinga.

Shtaka la saba na la mwisho lilisema Gavana Mwangaza alidharau Bunge la Kaunti. Shtaka hilo limepata uungwaji mkono kutoka kwa maseneta 10 pekee, tena wakilemewa na 37 waliopinga.

“Seneti haijathibitisha kosa lolote hivyo Gavana Kawira Mwangaza anaendelea kuongoza Kaunti ya Meru,” amesema spika Kingi.

Ikiwa maseneta wangepitisha hata shtaka moja tu, basi Gavana Mwangaza angebanduliwa ofisini.

Sasa cha kusubiriwa ni kuona namna atakavyojinyanyua tena na kutafuta njia ya kushirikiana na madiwani waliopitisha hoja ya kumbandua.

Hii imekuwa mara ya pili kwa kesi dhidi ya Gavana Mwangaza kuwasilishwa na kujadiliwa katika Bunge la Seneti.

  • Tags

You can share this post!

Demu mpenzi wangu ananyemelewa baa anakofanya kazi....

Wafanyabiashara mjini Kilifi wakerwa kufurushwa bila...

T L