• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Haji sasa atetewa na wabunge kutoka jamii za wafugaji

Haji sasa atetewa na wabunge kutoka jamii za wafugaji

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE kutoka jamii za wafugaji sasa wanadai kuwa baadhi ya mashirika ya kijamii yanaendesha njama ya kumpaka tope Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji anapokaribia kuhojiwa na wabunge kubaini ufaafu wake kwa wadhifa wa Mkurugenzi wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS).

Wakiongozwa na mdhamini wa muungano wa wabunge kutoka jamii hizo, Mbunge wa Sako Dido Rasso, wabunge hao walihoji sababu ya mashirika hayo kuibua pingamizi dhidi ya uteuzi wa Bw Haji lakini hayakufanya hivyo tangu 2018, afisa huyo alipoteuliwa katika wadhifa anaoshikilia sasa.

Bw Haji anatarajiwa kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi, Ujasusi na Mahusiano ya Kigeni kupigwa msasa kubaini ikiwa anafaa kuchukua nafasi ya Mkurugenzi wa NIS Philip Kameru anayestaafu. Atahojiwa saa nane mchana wa leo Jumanne.

Shirika la Kimataifa la kupambana na ufisadi, Transparency International (TI) linaongoza kampeni za kupinga uteuzi wa Bw Haji kwa wadhifa huo mkuu, likidai alivunja Katiba na sheria husika kwa kusitisha kesi nyingi za ufisadi zilizohusisha wanasiasa wandani wa Rais William Ruto kwa njia ya kutatanisha.

Miongoni mwa kesi hizo ni zile ambazo ziliwakabili Naibu Rais Rigathi Gachagua na mawaziri Aisha Jumwa (Utumishi wa Umma) na Mithika Linturi (Kilimo).

Mnamo Ijumaa wiki jana, shirika la TI-Kenya lilimvua Bw Haji tuzo ya uongozi na maadili ambayo lilimtunuku Bw Haji mnamo 2019.

Kwenye taarifa, shirika hilo lilisema kuwa imechukua hatua hiyo kufuatia maombi kutoka wadau mbalimbali wanaoshikilia kuwa Haji hajatimiza kiwango cha maadili hitajika kwa cheo cha Mkurugenzi Mkuu wa NIS.

“TI- Kenya imechunguza maombi hayo na kuamua kumpokonya Bw Haji tuzo ya maadili na uongozi iliyotolewa mwaka 2019. Hii ni kwa sababu wadau hao hawajaridhika na hatua ya DPP kuondoa kesi kubwa za ufisadi zilizochangia kupotea kwa pesa za umma,” ikasema taarifa iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa TI-Kenya Bi Sheila Masinde.

Shirika hilo lilimsuta Bw Haji kwa kushusha imani ya umma kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) hali ambayo inakwenda kinyume na hitaji la Sura ya Sita ya Katiba kuhusu maadili na uongozi na sheria zingine husika.

Lakini Jumatatu, Mei 29, 2023, Bw Rasso na wenzake walimtetea Bw Haji dhidi ya shutuma hizo wakisema kuwa alisitisha kesi hizo kutokana na ukosefu wa ushahidi tosha wa kuzihimili mahakamani.

“Katiba na sheria ya Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma inampa mshirikilizi wa cheo hicho mamlaka ya kusitisha kesi ikiwa atakosa ushahidi wa kutosha. Hiyo ndio hatua ambayo Haji alichukua,” Bw Rasso ambaye ni Mbunge wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

“Ni wajibu wa Rais kuteua mtu bora kwa wadhifa wa Mkurugenzi wa NIS. Kwa hivyo, Rais alimchagua Haji kuwa mshauri wake mkuu kuhusu masuala ya usalama baada ya kukagua ufaafu wake na kuridhika kwamba anafaa kwa kazi hiyo. Kwa hivyo, tunaonya mashirika ya kijamii dhidi ya kumchafulia jina Bw Haji wakati huu anapoelekea kuhojiwa na Kamati husika ya Bunge,” akaeleza Bw Rasso.

Kwa upande wake Mbunge wa Eldas Adan Keynan akasema hivi: “Ikiwa kuna masuala mengine kuhusu Haji huenda yakatokea baadaye. Lakini kufikia sasa Haji amefanyakazi mzuri. Suala la kufaulu kuwashtaka wafisadi haliko chini ya afisi yake. Uchunguzi hufanywa na polisi na kazi wa DPP ni kufungulia washukiwa mashtaka ikiwa kuna ushahidi wa kutosha.”

Kwa upande wake, Mbunge wa Turkana Magharibi Daniel Nanok alielezea matumaini kwamba licha ya pingamizi anazokabiliwa nazo Haji ndiye anayefaa kwa wadhifa huo.

“Sisi kama wabunge kutokana jamii za wafugaji, tuna imani kwamba Kamati ya Ulinzi, Ujasusi na Masuala ya Kigeni inayoongozwa na mwenzetu Mbunge wa Belgut Nelson Koech itaidhinisha uteuzi wake na kupendekeza kupitishwa kwake katika kamati ya bunge lote,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Vikwazo viondolewe kabla ya vitambulisho...

Stephen Lenamarle achaguliwa Spika mpya wa Samburu

T L