• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Hatimaye Rais Ebrahim Raisi atua nchini

Hatimaye Rais Ebrahim Raisi atua nchini

NA BENSON MATHEKA

Akiingia zulia jekundu na limetandazwa katika Ikulu kwa hafla hiyo. Mwenyeji wake Rais wa Kenya Dkt William Ruto amempokea mgeni huyo ambaye ameandaliwa gwaride rasmi na wanajeshi wa Kenya.

Maswali yaliibuka kuhusu maandalizi duni yaliyoaibisha serikali baada ya kulazimika kuahirisha ziara ya Rais wa Iran dakika ya mwisho kutoka jana Jumanne hadi leo Jumatano.

Mnamo Jumatatu, Ikulu ilituma mwaliko kwa vyombo vya habari kuomba wanahabari kufika Ikulu ya Nairobi kuangazia mkutano wa pamoja wa Rais William Ruto na kiongozi huyo wa Iran.

Barua ya mwaliko iliyotumwa na Katibu wa Habari katika Ikulu Emmanuel Talam ilisema, Rais Ruto na mgeni wake Rais Raisi, wangehutubia wanahabari jana Jumanne saa tatu asubuhi katika Ikulu ya Nairobi.

Kwa kawaida, mwaliko kama huo unatumiwa wanahabari baada ya ziara ya kiongozi wa nchi ya kigeni kuthibitishwa na maandalizi kukamilika.

Hata hivyo, wanahabari waliotumwa na kampuni zao walipofika katika lango la Ikulu kabla ya saa tatu jana asubuhi, walifahamishwa kuwa ziara ya kiongozi huyo wa Iran ilikuwa imeahirishwa.

Msemaji wa Ikulu Bw Hussein Mohammed aliambia wanahabari kwamba, ziara ya Rais Raisi ilikuwa imebadilishwa bila kutoa maelezo zaidi, hatua iliyozua mdahalo miongoni mwa Wakenya.

Baadhi walidai kwamba, serikali ilifuta ziara hiyo ili kupendeza mataifa ya Ulaya na Amerika ambayo kwa miaka mingi uhusiano wao na Iran umekuwa na doa.

Wengine walilaumu maafisa wa Ikulu na Wizara ya Mashauri ya Kigeni kwa kuaibisha kiongozi wa nchi kwa kufanya ziara ya kiongozi mwenzake kubadilishwa dakika za mwisho.

Haikubainika iwapo kulikuwa na maandalizi ya gwaride la heshima kutoka kwa vikosi vya usalama vya Kenya inavyofanyika kiongozi wa nchi anapozuru nchini.

Katika taarifa iliyoonyesha wazi aibu iliyosababisha ziara hiyo kuahirishwa dakika za mwisho, Waziri wa Mashauri ya Kigeni Dkt Alfred Mutua alisema ziara ya rais huyo iliahirishwa ili kupiga msasa Mikataba ya Maelewano kati ya nchi hizo mbili.

Dkt Mutua alieleza kuwa, Kenya na Iran zilikubaliana kuahirisha ziara hiyo hadi leo Jumatano lakini hakueleza kwanini hatua hiyo ilichukuliwa dakika ya mwisho hasa baada ya maandalizi kukamilika.

“Rais wa Iran, Mheshimiwa Ebrahim Raisi, alipangiwa kuwasili nchini kwa ziara leo (jana Jumanne). Ziara hiyo ilikuwa ya kupatia nchi hizi mbili fursa ya kuchunguza upya na kutia nguvu uhusiano wa kibiashara kwa manufaa ya watu wa nchi hizo mbili,” Dkt Mutua alisema kwenye taarifa.

Dkt Mutua alitangaza kuwa, Rais Raisi atawasili Ikulu leo saa moja asubuhi kufanya mazungumzo na Rais Ruto.

Maswali ambayo Wakenya wameuliza ni nani alifeli katika jukumu lake na kusababisha utepetevu wa kidiplomasia? Ni nani alifeli katika mawasiliano hadi kuabisha Rais na serikali yake?

Je, kuna afisa katika ikulu au wizara ya kigeni aliharakisha kutangaza ziara hiyo kabla ya kuiva? Ingawa awali, ziara ya rais huyo nchini ilitangazwa kuwa ya siku tatu, Dkt Mutua aliashiria kuwa huenda ikawa ya siku moja.

“Rais (wa Iran) atakuwa Ikulu saa moja asubuhi kwa mkutano. Baadaye, ataelekea katika kaburi la Hayati Mzee Jomo Kenyatta kuweka shada la maua kabla ya kuelekea nchi nyingine za Afrika,” alisema Dkt Mutua.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi watilia shaka usalama wao kambini Juhudi Primary

Mama wa watoto 6 kufanya KCSE 2023

T L