• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Wakazi watilia shaka usalama wao kambini Juhudi Primary

Wakazi watilia shaka usalama wao kambini Juhudi Primary

NA KALUME KAZUNGU

WAKIMBIZI waliotoroka mashambulio ya Al-Shabaab vijijini na ambao wamepiga kambi kwenye Shule ya Msingi ya Juhudi, kaunti ya Lamu wanadai hawapati usalama wa kutosha.

Jumla ya familia 207 kutoka vijiji vya Juhudi, Marafa, Salama, Mashogoni, Mavuno, Widho, Poromoko na viungani mwake wamekuwa wakipiga kambi na kulala kwenye shule ya Juhudi usiku kucha tangu magaidi wa Al-Shabaab walipovamia vijiji vyao na kuwachinja wanaume watano na kuteketeza nyumba sita Juni 24,2023.

Familia hizo hurudi vijijini mwao na kushinda mchana pekee.

Katika mahojiano na Taifa Leo, wakimbizi hao waliilaumu serikali kwa kukosa kuwajibikia ipasavyo suala la usalama kambini.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa siku za hivi karibuni, wakimbizi hao wamekuwa wakilindwa na polisi sita pekee wa akiba (NPR) hasa nyakati za usiku.

Aidha wanasema polisi wa kawaida hawawapi usalama jinsi walivyotarajia na hata wanajeshi hawajawapa ulinzi waliotarajia.

Simon Mwangi anasema kukosekana kwa KDF na polisi wa kawaida kambini humo ni suala lisiloridhisha na ambalo limekuwa likiwakosesha usingizi kila wakati.

Bw Mwangi alisema ni mara moja moja ambapo wao hupokea afisa mmoja au wawili wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Kibaoni kuwalinda.

“Kambi ina familia zaidi ya 200 ilhali tunalindwa na NPR sita pekee,” akasema Bw Mwangi.

Peter Githio,64, mkazi wa Salama na mmoja wa wakimbizi, alisema aliafikia kuhamia kwenye kambi ya Shule ya Msingi ya Juhudi akijua fika kuwa usalama pale ni wa uhakika.

Bw Githio anasema kupewa NPR sita pekee wa kuwalinda, hasa usiku si jambo la kuaminika au kuridhisha.

Aliirai serikali kuweka kambi za polisi na KDF vijijini mwao ili wavunje kambi na kurudi makwao kujiendeleza.

“Vijijini mwetu hatuko salama. Hapa kambini pia hatulindwi. Twahofia usalama wetu sasa. Serikali ifikirie kuweka kambi za KDF na polisi, ikiwemo GSU na RDU kwenye sehemu kama vile lango la Marafa-Juhudi na Juhudi-Salama. Haya ndiyo maeneo yanayotumiwa sana na magaidi kuvamia vijiji vyetu. Wakibuni hizo kambi za usalama sisi tutakuwa na uhakika wa usalama wa maisha na mali,” akasema Bw Githio.

Bi Mary Wanjiru, mkazi wa kijiji cha Marafa, anasema anavumilia kuishi kambini akijua fika kuwa chochote kinaweza kutokea kwani usalama bado ni finyu kambini.

“Kila wanapozuru eneo hili wanatuambia usalama umedhibitiwa na turudi vijijini mwetu. Tutarudije vijijini iwapo hata hapa kambini tayari usalama hawawezi kuweka wa kutosha? Serikali iache mchezo,” akasema Bi Wanjiru.

Kauli ya wakimbizi hao inajiri siku chache baada ya Katibu Mkuu katika Wizara ya Matangazo, Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Abubakar Hassan, kuzuru kambi ya Juhudi na kuwaahidi wakazi kwamba atazungumza na katibu mwenza wa usalama wa Ndani ili kuhakikisha usalama wa kutosha unawekwa vijijini.

Bw Hassan, ambaye ni mzaliwa wa Lamu, alizuru kambi hiyo akiwa ameandamana na wakuu wa usalama wa Lamu wakiongozwa na Kamishna wa eneo hilo, Louis Rono na Kamanda wa Polisi wa Lamu, William Samoei.

Hivi majuzi, Bw Rono alizomewa na wakimbizi hao pale alipowashurutisha kuvunja kambi na kurudi vijijini mwao, akishikilia kuwa serikali imedhibiti usalama mashambani.

Hadi sasa, wakimbizi wamedinda kuondoka kambini.

Juhudi za kumpata kamishna Louis Rono kuzungumzia suala la usalama wa wakimbizi kwenye kambi ya Juhudi ziligonga mwamba kwani simu yake haikupokelewa.

  • Tags

You can share this post!

Katibu aliyeshtakiwa kumpiga mke mbele ya watoto ana kesi...

Hatimaye Rais Ebrahim Raisi atua nchini

T L