• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Mama wa watoto 6 kufanya KCSE 2023

Mama wa watoto 6 kufanya KCSE 2023

NA TITUS OMINDE

AKIWA na umri wa miaka 12, Esther Khamala alijikuta katika ndoa ambayo hakutarajia.

Mwenyewe anadai mwanamume aliyejifanya malaika aliyetumwa na Mungu kumwokoa kutoka kwa wajomba wake waliokuwa wakimnyanyasa baada ya kufariki kwa nyanyake aligeuka kuwa mwindaji.

“Nilipokutana na mtu huyu alionekana kuwa mzuri kwangu, nilikuwa nikitafuta mtu ambaye atanisaidia kutimiza ndoto ya kwenda shule na kufikia lengo la kuwa na maisha mazuri,” anasema Bi Esther ambaye sasa ana umri wa miaka 40 na Mtahiniwa wa KCSE katika shule ya Sekondari ya Matunda SA katika kaunti ndogo ya Likuyani.

Bi Esther ambaye hajawahi kumuona mama yake mzazi, alilelewa na nyanyake mzaa mama lakini mambo yalibadilika akiwa na umri wa miaka 12 bibi huyo alipofariki.

Baada ya kufunga ndoa isiyotarajiwa akiwa na umri wa miaka 12, alijifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume mnamo 1994 akiwa na umri wa miaka 13.

“Nilikutana na mwanamume ambaye aliharibu maisha yangu mwaka wa 1994. Alikuwa amenihakikishia kuwa wazazi wake wataniunga mkono nirudi shuleni kwani nitakuwa nikifanya kazi ya nyumbani kwa familia hiyo huku wakinilipia karo. Mambo yalibadilika haraka kabla sijagundua nilikuwa mke wa mwanamume huyo aliyekuwa na umri wa miaka 20 baada ya kujifungua mtoto wangu wa kwanza wa kiume mwaka huo huo,” anasema Esther ambaye sasa ni mama wa watoto sita.

Analalamika kwamba baada ya kuzaa watoto sita, mwanamume huyo aligeuka kuwa jeuri kwa sababu ya uraibu wa pombe na akauza ardhi ya familia nzima akimuacha bila matumaini.

Juhudi zake za kutafuta msaada kutoka kwa wakwe hazikuzaa matunda kwa vile wakwe zake wote walikuwa kinyume chake, wakimtaja kuwa mwanamke asiyejua kusoma na kuandika ambaye hakustahili kuolewa na mwana wao aliyesoma.

Esther Khamala akiondoka shuleni baada ya masomo. PICHA | TITUS OMINDE

Pia anasema kuwa ukabila pia ulichangia katika mizozo ya familia yake.

Jaribio lake la kuokoa mali ya familia ambayo iliuzwa na mumewe wakati huo lilimpeleka rumande kwa miaka mitatu baada ya kushtakiwa kwa wizi wa kutumia nguvu.

Hata hivyo, mahakama ya Kitale ilimwachilia kwa kukosa ushahidi wa kumfunga jela.

“Nilikaa rumande kwa miaka mitatu kwa kosa ambalo sikufanya. Nilikuwa nikipigania tu mali ya familia yangu ambayo iliibuka kuwa mashtaka ya wizi wa kutumia nguvu. Ninamshukuru Mungu kuwa hakimu aliyeniachilia baada ya kupatikana bila hatia kwa madai ya uhalifu,” akasema Bi Esther.

Alipoachiliwa kutoka gerezani mwaka 2009, aliamua kujiunga na shule ya msingi huko Matunda.

Mnamo 2019 alifanya mtihani wake wa KCPE na kupata alama 290 na mwaka huo huo mwanawe akafanya mtihani sawa na kupata alama 378.

Mama na mwanawe wanafanya KCSE mwaka huu wa 2023. Mwanawe alipata ufadhili kutoka benki ya Equity ambapo analipiwa karo katika Shule ya Upili ya Butula katika Kaunti ya Busia.

Kitindamimba wake aliyefanya KCPE 2022 na kupata alama 349 yuko Kidato cha Kwanza katika shule ambayo mama huyo anasomea.

Bi Esther anasema wakati wa likizo, yeye hufanya kazi zisizo za kawaida kusaidia watoto wake.

Hivi sasa wanawe watatu wakubwa wamekamilisha elimu yao ya sekondari na ambapo wanafanya kazi za juakali katika miji tofauti.

Anasema mwanawe mkubwa alikosa kujiunga na jeshi (KDF) kutokana na kile anasema ni ufisadi. Kisa hicho kimemfanya achukie ufisadi na kutojua kusoma na kuandika.

“Mwanangu ambaye alikuwa amefuzu kutoka NYS alikosa fursa ya kujiunga na KDF kutokana na ukabila na ufisadi. Nataka kupata elimu ambayo itanisaidia kupambana na ufisadi katika nchi yetu kwa njia zote,” anajipa ari.

Licha ya changamoto mbalimbali anazokabiliana nazo zikiwemo tatizo la kulipa kodi ya nyumba anayotarajia kufanya vyema katika KCSE mwaka huu.

Mapema mwaka 2023 alipata msaada kutoka kwa wasamaria wema waliomlipia sehemu ya karo yake ya shule.

“Namshukuru Mungu kwa mfadhili aliyejitolea kunilipia karo ya shule hapa Matunda SA Sekondari. Changamoto yangu kubwa ni malipo ya kodi ya nyumba kwa vile ninakaa na watoto wangu kwenye nyumba ya kupanga katika Mji wa Matunda. Tunapozungumza tayari nimepokea notisi ya kufukuzwa kwa sababu ya kutolipa kodi kwa zaidi ya miezi mitano,” anasema Bi Esther.

Bi Esther anasimulia kwamba aliamua kurejea shuleni kutokana na changamoto ambazo alikuwa akikabiliana nazo maishani na kugundua kuwa changamoto hizo zilitatuliwa kwa urahisi na watu waliosoma.

“Katika maisha yangu, nimegundua kuwa watu waliosoma hutatua masuala yao kwa urahisi na kwa njia bora zaidi na hiyo ndiyo sababu mojawapo iliyonilazimu kurejea shuleni licha ya umri huu mkubwa,” anaeleza.

Anasema licha ya changamoto anazokabiliana nazo, ana matumaini ya kufaulu katika KCSE na kujiunga na chuo kikuu kusomea taaluma inayojikita katika kuangazia haki za kijamii ili kuwalinda wanaokandamizwa katika jamii.

Anapania kuwa mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu.

Walimu wake wamempongeza kwa ustahimilivu, nidhamu na kujitolea kwa elimu yake.

Shuleni anafanya kazi maradufu kama vile kumotisha wanafunzi wenzake na vile vile kuwapa ushauri nasaha.

“Yeye ni mfano mzuri kwa wanafunzi wengine. Wakati wake wa kupumzika, husaidia kama mshauri wasichana wetu. Amewapa motisha wengi wao,” anasema mwalimu mkuu wa Matunda SA Bi Mary Luvanda.

Bi Luvanda anasema alimkubali Bi Esther kutokana na unyenyekevu na kiu yake ya kupata elimu.

Bi Esther Khamala akiandika. PICHA | TITUS OMINDE

Bi Luvanda anakumbuka kwamba mara ya kwanza aliposikia hadithi ya Bi Esther, alitokwa na machozi.

 “Tangu ajiunge na shule hii amekuwa mfano wa kuigwa na wasichana wengine kutokana na uzoefu wake alipokuwa mama kijana katika umri mdogo. Kutokana na hadithi yake ya maisha anawahimiza wanafunzi wengine katika shule yangu kuthamini elimu,” anasema Bi Luvanda.

Bi Luvanda anaongeza kwamba ingawa Bi Esther anakabiliwa na baadhi ya changamoto kutoka kwa wanafunzi wadogo ambao wakati mwingine wanamdharau, mara kwa mara amekuwa na ujasiri wa kukabiliana na changamoto hiyo kwa kusisitiza kwamba lazima asome na ahitimu katika KCSE.

“Wakati mwingine hukosa shule kwa karibu wiki mbili kutokana na changamoto za kuwa mama lakini kama shule tunaelewa hali yake,” anasema Bi Luvanda.

Bi Luvanda anawashukuru wahisani ambao wamemuunga mkono Bi Esther kwa kumlipia karo.

Bi Luvanda anatoa changamoto kwa wakuu wengine kuwa tayari kusaidia wanafunzi kama hao katika shule zao akisema wanafunzi kama hao hupitia wakati mgumu sana na wanahitaji upendo na mwelekeo wa kuwawezesha kuendelea.

  • Tags

You can share this post!

Hatimaye Rais Ebrahim Raisi atua nchini

Shughuli za kawaida zatatizwa na maandamano, mgomo wa...

T L