• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kamanda wa GSU kuapishwa Naibu Inspekta Jenerali

Kamanda wa GSU kuapishwa Naibu Inspekta Jenerali

NA SAMMY WAWERU 

KAMANDA wa Kikosi cha askari kukabiliana na ghasia (GSU), Douglas Kanja Kirocho ndiye Naibu Inspekta Jenerali (DIG) mpya wa Polisi nchini kitengo cha askari wa kawaida, KPS.

Bw Kanja amemrithi Edward Mbugua, aliyestaafu mwezi uliopita, Machi.

Afisa huyo ataapishwa kesho, Alhamisi kuanza kutekeleza rasmi majukumu yake kama DIG.

Ikulu ya Rais, Jumatano ilitangaza kuteuliwa kwa Kanja na Rais William Ruto.

Aidha, jina la afisa huyo lilikuwa miongoni mwa majina matatu yaliyowasilishwa kwa Rais na Tume ya Huduma za Polisi Nchini (NPSC) baada ya zoezi la mchujo kufanyika.

Ikulu ya Rais pia ilitangaza mabadiliko katika huduma polisi, ambapo aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchunguzi Idara ya Uchunguzi wa Jinai na Uhalifu (DCI) Eliud Kipkoech aliteuliwa kuwa Kamanda mpya wa GSU.

Kupitia Notisi ya Gazeti Rasmi la Kiserikali, Rais Ruto pia alimteua aliyekuwa Msemaji wa Polisi na Kamanda wa Chuo cha Mafunzo ya Askari Kiganjo, Bruno Shioso kama Mkurugenzi Mkuu Kenya Coast Guard Service.

Bw Shioso atahudumu katika kitengo hicho muda wa miaka minne.

Mabadiliko mengine katika NPS, Gideon Munga Nyale ambaye amekuwa akihudumu kama Mkurugenzi wa Mikakati katika Idara ya Polisi alipandishwa ngazi kuwa Kamanda Chuo cha Mafunzo ya Askari Kiganjo.

Ranson Lolmodoni naye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mikakati NPS.

  • Tags

You can share this post!

Kesi: Wizi wa watoto Mama Lucy

Gachagua apinga handisheki akisaka ubabe Mlima Kenya

T L