• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Kamati maalum ya Seneti yaanza uchunguzi kutegua kitendawili cha vifo Shakahola

Kamati maalum ya Seneti yaanza uchunguzi kutegua kitendawili cha vifo Shakahola

NA ALEX KALAMA 

KAMATI maalum iliyobuniwa na bunge la Seneti imeanza rasmi uchunguzi wake ili kutegua kitendawili cha vifo vya waumini wa dhehebu tata la Good News International kwenye msitu wa Shakahola katika Kaunti ya Kilifi.

Kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Seneti Amason Kingi imefika Shakahola kudadisi hali ilivyo siku chache baada ya shinikizo kwa serikali ibuni sheria za kudhibiti nyumba za kuabudu nchini.

“Nimekuwa mbunge wa eneo hili, nimekuwa gavana wa eneo hili lakini hakuna siku nilipata ripoti kuhusu mauaji ya Shakahola kwa sababu Paul Mackenzie amekuwa akiendesha mambo yake kwa usiri bila kuhusisha wakazi,” amesema Spika Kingi.

Hata hivyo Kingi ameilaumu idara ya mahakama kwa kutowajibikia kesi dhidi ya mhubiri huyo.

“Mackenzie ameshikwa mara nyingi na kupelekwa mahakamani lakini cha kushangaza ni kwamba amekuwa akiachiliwa tu kwa urahisi licha ya kwamba madhara ambayo amekuwa akiiletea jamii ni makubwa. Safari hii tunataka mahakama iwajibike,” akasema.

Operesheni ya kuwatafuta wafuasi wa dhehebu la Good News International imeshika kasi msituni Shakahola huku maafisa wa polisi wakilenga maeneo ambayo yanaaminika kuwa na idadi kubwa ya watu ambao bado wako kwenye mfungo.

Baadhi ya wanachama wa kamati ya seneti inayochunguza matukio kwenye chaka la mauti la Shakahola. PICHA | WACHIRA MWANGI

Kikosi cha maafisa kinachoendeleza operesheni hiyo na ambacho kinaongozwa na Martin Nyuguto mnamo Jumamosi kiliwapata watu wanne wakiwa wangali hai katika shamba linalodaiwa kuwa la mhubiri Mackenzie.

“Leo tumeokoa watu wanne lakini kwa bahati mbaya mmoja – wa tano – amepatikana ameaga dunia,” amesema Bw Nyuguto.

Operesheni hiyo imepigwa jeki na ndege zinazoshika doria angani, licha ya hofu kwamba huenda waathiriwa wamehamishwa hadi maeneo mapya eneo hilo.

Hata hivyo, idadi ya manusura imefika watu 45 huku idadi ya wahanga walioangamia ikiongezeka hadi 110.

Upasuaji na uchunguzi wa maiti zilizofukuliwa Shakahola utaanza wiki ijayo.

  • Tags

You can share this post!

Vihiga Queens sasa wadhibiti jedwali KWPL

BAHARI YA MAPENZI: Uvumilivu ni mzuri ila nao una mipaka

T L