• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:21 PM
BAHARI YA MAPENZI: Uvumilivu ni mzuri ila nao una mipaka

BAHARI YA MAPENZI: Uvumilivu ni mzuri ila nao una mipaka

NA BENSON MATHEKA

NDOA ni kuvumiliana na bila uvumilivu ndoa haiwezi kufaulu.

Kuvumilia kunamaanisha kukubali hali mbaya na ngumu ambazo hazifurahishi mtu.

Hasa, hali hizi huwa ni ngumu na nzito sana zinazoumiza mtu. Ni hali ambazo mtu huwa hakuwa amezoea kabla ya kuingia katika ndoa au kutarajia kupata katika ndoa. Baadhi ya shida huwa zinasababishwa na mchumba wake au kuzuka kutokana na hali ambazo haziepukiki. Mtu pia anaweza kusababisha hali ngumu katika ndoa yake.

Ingawa wanandoa wanafaa kuvumiliana, kiwango cha uvumilivu na mipaka yake pia kinapaswa kuzingatiwa.

Kuna shida zinazoweza kuvumiliwa kwa muda mrefu hadi hali ibadilike na kuwa bora na kuna zile ambazo hata zikivumiliwa mtu hawezi kupata afueni. Wakati mwingine watu huwa wanavumilia hali ambazo zinawaweka kwenye hatari na kwa kufanya hivyo uvumilivu wao huwa wa upofu.

Kuvumilia mume au mkeo akiwa mgonjwa au akipoteza kazi ni jambo nzuri na la kupongezwa. Hii ndiyo aina ya uvumilivu wa kiapo cha ndoa.

Huu ni uvumilivu unaotokana na mapenzi ya dhati, pale mume na mke wanasaidiana huku wakipitia hali ngumu ya uchumi na maradhi. Itakuwa kukiuka kiapo cha ndoa iwapo sio ukatili mtu kuacha mumewe au mkewe akiwa mgonjwa akisema amekuwa mzigo kwake. Lakini hii ni tofauti na mtu kuvumilia mtu anayemtesa kimakusudi hima kimwili au kisaikolojia. Kuna watu wanaovumilia kushambuliwa kimwili na kisaikolojia na wachumba wao hadi wanaathirika kiafya na hata kulemazwa. Kuvumilia mateso ya aina hii ni kilele kikubwa cha upumbavu.

Kuna wanaume na wanawake wanaovumilia mateso kutoka kwa wachumba wao hadi kaburini na kuwaacha waliowatesa wakiendelea na maisha.

Katika kisa kimoja, mwanamke alivumilia madharau ya mumewe kuwaleta wanawake tofauti kulala nao katika kitanda cha ndoa huku akiamrishwa kulala kwenye kochi. Hatimaye mwanamume huyo aliambukizwa Ukimwi na kufariki akiwa amepitisha kwa mkewe. Kama mwanamke huyo hangevumilia kijinga na kujiondoa katika ndoa, pengine hangejipata katika hali ya kuhuzunisha ya kuachwa mjane anayeishi na Ukimwi.

Hata kama uvumilivu ni muhimu katika ndoa, unafaa kukitwa kwa busara na hekima, haufai kuwa wa kienyeji tu eti kwa kuheshimu kiapo cha ndoa. Itakuwa ujinga kuheshimu kiapo cha ndoa yako na mtu ambaye hakiheshimu na hakuheshimu.

Vumilia ndoa yako na mtu anayekuheshimu lakini usivumilie katili anayeweza kukupeleka kaburini na kuachwa akiendelea kufurahia maisha yake kana kwamba haukuwahi kuwa katika maisha yake au katika dunia hii.

Maisha ni yako na yake ni yake, kinachowaunganisha ni upendo na kukutumbukiza katika mateso kunaonyesha upendo wake kwako umetoweka.

Mambo ni mawili; waume wapende wake zao, wawajibike na kuheshimu ndoa iwapo wanataka wawavumilie hali ngumu zinapozuka. Wake nao waheshimu waume zao hata wakiwa wadhaifu na katika mazingira haya ndoa zidumu na kuwa na furaha.

  • Tags

You can share this post!

Kamati maalum ya Seneti yaanza uchunguzi kutegua...

JUNGU KUU: Ruto atarajie presha kali kutoka kwa Raila

T L