• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Kikosi kipya kuweka ulinzi uchaguzini

Kikosi kipya kuweka ulinzi uchaguzini

Na GEORGE MUNENE

SERIKALI itabuni kikosi maalum cha walinda usalama kitakachoshirikisha machifu kudumisha usalama kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu.

Katibu katika Wizara ya Usalama, Dkt Karanja Kibicho, alisema mipango ya kuundwa kwa kikosi hicho iko katika hatua ya mwisho.

Dkt Kibicho aliwahakikishia Wakenya kwamba uchaguzi mkuu ujao utaendeshwa katika mazingira salama zaidi.

Katibu huyo ambaye alikuwa akiwahutubia maafisa wa usalama mjini Kagio, kaunti ya Kirinyaga alisema tayari serikali imetambua maeneo hatari ili kudhibitisha uwezekano wa kutokea kwa ghasia.

“Wakenya wasiwe na wasiwasi wowote kwa sababu mipango ya usalama imewekwa kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unaendeshwa katika mazingira huru na yenye amani,” Dkt Kibicho akaeleza.

Alikariri kuwa wahalifu ambao hukodiwa kuvuruga mikutano ya kisiasa watakabiliwa ipasavyo.

“Tutapambana vikali na magenge ya wahalifu ambao watajaribu kuleta machafuko nchini,” Dkt Kibicho akasema huku akiwaamuru machifu, makamishna wa kaunti na maafisa wa polisi kuhakikisha Wakenya wanawachagua viongozi wanaowataka kwa amani Agosti 9, 2022.

Katibu huyo aliahidi kuwa manaibu kamishna wa kaunti wote watapewa magari rasmi ili kuwasaidia kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Manaibu wa makamishna wa kaunti hawawezi kufanya kazi ipasavyo bila magari. Kwa hivyo, serikali itatoa magari hayo na vifaa vinginevyo hitajika,” Dkt Kibicho akasema.

Aliongeza kuwa serikali ina maafisa tosha wa polisi wenye uwezo wa kuzuia uwezekano wa kutokea kwa ghasia zozote kipindi cha kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu.

Dkt Kibicho alilalamika kuwa shughuli ya utengenezaji pombe haramu zimeanza kurejelewa katika sehemu mbalimbali nchini.

Alisema mwenendo wa utengenezaji na unywaji wa pombe haramu unaathiri shughuli za maendeleo nchini.

“Kwa hivyo, nawaamuru machifu kote nchini kuendelea kupambana na utengenezaji wa pombe haramu,” akasema Dkt Kibicho.

  • Tags

You can share this post!

Kocha Klopp kukosa gozi la EPL kati ya Liverpool na Chelsea...

UDAKU: Essien na mkewe Akosua Puni wamerejesha tena mahaba

T L