• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Kilio cha familia ya kijana aliyetoweka alipoenda kumtembelea mpenziwe Desemba 2021

Kilio cha familia ya kijana aliyetoweka alipoenda kumtembelea mpenziwe Desemba 2021

NA MERCY KOSKEI

NI miaka miwili sasa tangu Bw Abraham Mogaka Mogere alipotoweka kwa njia tatanishi baada ya kutoka nyumbani kwao katika eneo la 58, Kaunti ya Nakuru.

Kulingana na ndugu yake Felix Ogero, Bw Mogaka Mogere alitoweka Desemba 13, 2021, baada ya kueleza familia yake alikuwa na shughuli mjini Nakuru (sasa jijini Nakuru).

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Egerton hakurejea nyumbani jioni hiyo. Isitoshe, hakuweza kupatikana kwa simu, hali na matukio yalioacha familia yake na hofu na maswali mengi.

Muda huu wote tangu kutoweka kwake, familia yake inaendelea kumtafuta kila mahali kwa matumaini ya kumpata ili aungane tena nao.

Mara nyingi juhudi zao zimekuwa zikiambulia patupu.

Bw Ogero alieleza Taifa Leo kuwa walizungumza na nduguye mara ya mwisho Desemba 11, 2021, saa nane mchana alipokuwa akiuliza alikoweka funguo za nyumba.

Alisema kuwa walipozungumza, kakake alikuwa na furaha kwani alikuwa anapanga kukutana na mchumba wake.

“Kipindi hicho nilikuwa jijini Mombasa alipopotea. Tulizungumza mara ya mwisho na kuniuliza nitarudi Nakuru lini kwani tulikuwa tunapanga mikakati ya kutembelea wazazi katika Kaunti ya Kisii kwa sherehe za Krismasi,” alisema.

Hata hivyo, baada ya siku mbili Bw Ogero alitamatisha shughuli za biashara Mombasa na  kurejea nyumbani. Alipokea taarifa ya kusikitisha kwamba Bw Mogere alikuwa ametoweka nyumbani.

“Imekuwa safari ngumu kwa familia ya kumtafuta kaka yangu. Inasikitisha kuwa wakati mwingi huwa namuwaza. Kupotea kwake kunafanya naumwa sana haswa wakati wa hafla za kifamilia kwa sababu kila mtu huuliza aliko, marafiki wake pia humuulizia. Unabaki tu na maswali ikiwa yuko sawa… ikiwa yuko hai bado,” alisema.

Bw Ogero alisema kuwa wametembelea hospitali na hifadhi ya maiti ya Nakuru Level 5, makafani ya Nakuru City na gereza la Nakuru GK ila hawajafanikiwa kumpata au mwili wake.

“Tumekuwa tukitembelea vyumba vya kuhifadhia maiti popote wanapotangaza kuwa wana miili ya watu wasiojulikana lakini hatujawahi kumpata. Tumefika kwa Mto Yala hasa wanapopata miili majini lakini juhudi zetu hazijazaa matunda yoyote,” alisimulia.

Kwa sasa familia hiyo ina matumaini kuwa maafisa wa usalama watawasaidia kumtafuta na pengine kumrejesha nyumbani.

  • Tags

You can share this post!

Mpenzi aliniacha kwa kumtamani rafikiye; nishauri sababu...

Kaunti ya Marsabit yaomba chopa, msaada wa chakula watu...

T L