• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Mto Tana wavunja kingo mafuriko yakitatiza shughuli za uchukuzi katika eneo la Gamba

Mto Tana wavunja kingo mafuriko yakitatiza shughuli za uchukuzi katika eneo la Gamba

NA KALUME KAZUNGU

SHUGHULI za uchukuzi zimekatizwa katika eneo la Gamba kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen baada ya maji ya mafuriko kuzagaa katika barabara hiyo mnamo Jumamosi.

Mafuriko hayo yamechangiwa na Mto Tana kuvunja kingo zake ghafla kutokana na mvua ya El-Nino inayoendelea kunyesha katika maeneo ya nyanda za juu.

Zaidi ya magari 50 ya uchukuzi wa umma, yakiwemo mabasi na matatu na hata magari ya kibinafsi yaliyokuwa yametoka Lamu kuelekea jijini Mombasa, yalilazimika kugeuza safari kurudi na kupakishwa mjini Witu kusubiri iwapo mafuriko yatapungua na kuruhusu safari kuendelea.

Gari dogo eneo la Gamba kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen. PICHA | KALUME KAZUNGU

Mamia ya abiria walisalia wasijue cha kufanya baada ya kushuhudia mafuriko hayo, hasa katika eneo ambalo hawakudhania yangeweza kutokea.

“Nilikuwa nimerauka kuabiri gari kuelekea mjini Mombasa kumuona daktari. Nilifaa nimuone saa nane na sasa bado nipo hapa Witu kusubiri hali ya kawaida kurejea katika barabara hiyo. Hii inamaanisha kuwa miadi yangu na daktari haitawezekana leo wala kesho kwani sijui maji yatapungua saa ngapi ili kuruhusu safari yetu kuendelea,” akasema Bi Betty Waweru.

Naye Bi Halima Abdallah anasema alikuwa akisafiri kuelekea mjini Malindi kwa hafla ya harusi ya mtoto wa dadake.

Anasema hana la kufanya kwa sasa kwani safari yake imekatizwa kutokana na mafuriko yaliyosomba barabara eneo la Gamba.

“Sijakula tangu niamke. Nimeraukia safari nikijua fika kwamba kufikia saa tano asubuhi ningekuwa mjini Malindi. Ni masikitiko kwamba safari imekatizwa. Sina senti za matumizi kula hapa mjini Witu ambapo magari yamepakiwa kusubiri mafuriko yapungue. Allah (Mungu) atusaidie,” akasema Bi Abdallah.

Katika kituo cha polisi cha Gamba, maji pia yalikuwa yameanza kufikia baadhi ya nyumba za polisi kuishi.

Si mara ya kwanza kwa kituo cha polisi cha Gamba kuathiriwa na mafuriko kila wakati mvua iliyopitiliza inaposhuhudiwa nchini.

Mmoja wa makondakta wa mabasi ya usafiri wa umma, Bw Said Swaleh alisema yeye pia amelazimika kusalia mjini Witu na makumi ya abiria wake baada ya basi lao kushindwa kuvuka eneo la Gamba kutokana na mafuriko hayo.

“Tumegeuza gari kurudi mjini Witu. Barabara haivukiki eneo la Gamba. Maji yametapakaa kila mahali na ni hatari kwetu kuvukisha gari. Twasubiri hadi mafuriko yapungue,” akasema Bw Swaleh.

Hali ilikuwa ile ile kwa wahudumu wa uchukuzi kutoka Malindi na Mombasa wakielekea Lamu kwani walilazimika kugeuza magari yao na kuyapakisha eneo la Minjila baada ya kushuhudia mafuriko eneo hilo la Gamba.

“Wa kutoka Lamu kuelekea Mombasa na yule wa Mombasa kuelekea Lamu, wote hawawezi kuvuka kutoka Gamba na kufululiza kwa safari zao. Hali ni mbaya hapa. Maji yamefurika kwelikweli eneo hili na ni hatari kwetu kuyavuka,” akasema Bw Paul Kariuki ambaye ni dereva wa probox.

  • Tags

You can share this post!

Familia yaamini jeneza lililotupwa barabarani ni la mpendwa...

Watu watano wapoteza maisha kwenye ajali mjini Molo

T L