• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Maandalizi ya Eid-ul-Adha yashika kasi

Maandalizi ya Eid-ul-Adha yashika kasi

NA KALUME KAZUNGU

WAISLAMU katika Kaunti ya Lamu wanazidi kujiandaa kuadhimisha sikukuu ya Eid-Ul-Adha juma hili huku wakilalamikia gharama ya juu ya maisha.

Sikukuu ya Eid-Ul-Adha huadhimishwa na waumini wa dini ya Kiislamu ulimwenguni kote, ambapo sana huandamana na kutoa kafara au kuchinja mifugo ikiwemo mbuzi, kondoo na ng’ombe.

Ni siku ambayo waumini wa dini ya Kiislamu huitumia kukumbuka kitendo cha Imani ambapo Nabii Ibrahimu alitaka kumtoa kafara mwanawe Ishmael kama alivyoamriwa na Allah, lakini akapewa kondoo na Mungu amtoe kafara badala yake.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Imamu wa Msikiti wa Jamia eneo la Mokowe, Kaunti ya Lamu, Mohamed Bwanamkuu ameshukuru Maulana kwa kuwafikisha wakati huu wa Eid-Ul-Adha, akiwasihi waumini kusaidia wengine wasiojiweza katika jamii kupitia kutoa sadaka licha ya uchumi mgumu unaoshuhudiwa nchini.

Kulingana na Bw Bwanamkuu, awali walikuwa wakinunua mbuzi au kondoo mmoja kwa Sh4,000 pekee.

Kupanda kwa gharama ya maisha hata hivyo kumeongeza bei ya mifugo, ambapo mbuzi au kondoo mmoja kwa sasa ananunuliwa kwa kati ya Sh6,000 hadi Sh7,000.

Bw Bwanamkuu amesisitiza haja ya watu kuonyesha upendo kwa kila mmoja.

“Licha ya ugumu wa maisha unaokabili Wakenya, ni vyema tujitahidi kusaidiana. Wale waliojaliwa wasaidie wengine. Ninatarajia tukichinja pia tugawanyie wale wasio na uwezo, hata kama watakuwa wengine si Waislamu. Tukifanya hivyo tunazidisha umoja, upendo na uwiano, hivyo kupata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu,” akasema Bw Bwanamkuu.

Bw Abubakar Athman ambaye ni muuzaji mifugo amesema ugumu wa maisha umepunguza idadi ya mbuzi na kondoo ambao yeye amekuwa akiuza kila mara kunapokuwa na sherehe.

“Mwaka 2022 niliuza karibu mbuzi na kondoo 100 na nikapata faida kubwa. Mwaka huu pale ninaponunua mifugo hiyo nimekuta wamepandisha bei. Nimezoea kununua mbuzi kwa Sh3,500. Nikisafirisha mimi huuza mbuzi au kondoo kwa Sh4,000 au Sh5,000 na ninapata faida nzuri. Sasa ikiwa tayari ninauziwa mbuzi Sh5,000 au Sh5,500. Nikisafirisha hadi wafike Lamu, nitauza kwa pesa ngapi ili nijipatie faida? Imebidi kununua mbuzi wachache kuwasafirisha kisiwani Lamu na wanunuzi pia wateja wa mbuzi wangu pia wamepungua,” akasema Bw Athman.

Ikumbukwe kuwa sikukuu ya Eid-Ul-Adha huadhimishwa kuanzia siku ya 10 tangu kuonekana kwa mwezi wa Dhu al-Hijjah.

Serikali tayari imetangaza siku ya Jumatano, Juni 28, 2023 kuwa siku ya mapumziko kuadhimisha sherehe za Eid-Ul-Adha.

Mbuzi wakikusanywa kwenye jeti ya Mokowe, Kaunti ya Lamu tayari kusafirishwa kwa boti kuelekea kisiwani Lamu mnamo Jumanne, Juni 27, 2023 ili kuchinjwa kwa maadhimisho ya sikukuu ya Eid-Ul-Adha. Kisiwa cha Lamu ni ngome ya Uislamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Ni wakati wa sikukuu hiyo ambapo Waislamu pia huvalia mavazi yao mazuri na ya kupendeza na kwenda msikitini kwa maombi.

Siku hiyo Waislamu hula chakula chenye nyama na huwapa jamaa, majirani na maskini nyama ya mnyama waliyemchinja.

Katika baadhi ya mataifa na miji, hairuhusiwi watu kuwachinja wanyama kwao nyumbani, hivyo vichinjio hutumiwa.

Waislamu pia hutoa pesa za hisani kipindi hiki cha Sikukuu ya Eid-Ul-Adha.

  • Tags

You can share this post!

Shakahola: Yabainika miili 117 kati ya 338 ni ya watoto

Modric sasa kuchezea Real Madrid hadi Juni 2024

T L