• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 7:00 AM
Machifu na wakuu wa askari watakaoshindwa kuzima pombe haramu kufutwa kazi

Machifu na wakuu wa askari watakaoshindwa kuzima pombe haramu kufutwa kazi

NA SAMMY WAWERU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ametoa onyo kali kwa wakuu wa polisi na machifu, akisema watumishi watakaolemewa kuzima kero ya pombe haramu watapigwa kalamu.

Bw Gachagua alisema Jumatatu, Mei 29, 2023 kuwa serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto haina nafasi ya watumishi wazembe na wasiofuata maagizo yanayolenga kuokoa taifa.

Akizungumza katika Kaunti ya Nakuru ambapo alikutana na viongozi wa kisiasa na wakuu wa polisi Bonde la Ufa, alisema atakapoandaa mkutano na umma kisha kuwe na mwananchi aliyekunywa pombe, mkuu wa askari anayesimamia eneo hilo na chifu watamwaga unga.

“Nikihudhuria mkutano halafu kuwepo na mwananchi aliyekunywa pombe, afisa msimamizi wa polisi eneo hilo na chifu wataenda nyumbani,” alitahadharisha.

Aliwataka wakuu wa polisi kuwa waaminifu katika utendakazi wao, akisisitiza wasikubali kupokea hongo ili kuachilia wauzaji wa pombe haramu au wanaotengeneza.

Bw Gachagua alitumia jukwaa hilo kuahidi askari kuwa serikali itaboresha maslahi yao, kimalipo na makao.

“Tulipounda jopokazi linaloongozwa na David Maraga kuangazia maslahi ya polisi, wananchi walipendekeza muongezewe mshahara ili muache kuitisha kitu kidogo. Hatuwezi tukampa kitu kikubwa kisha muendelea kuitisha kitu kidogo,” alielezea.

Kwa muda mrefu, askari wamekuwa wakilalamikia malipo na mazingira duni.

Bonde la Ufa limejiunga na Mlima Kenya katika vita dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua: Ni heri nipoteze umaarufu kuliko kuruhusu vijana...

Mahakama yaidhinisha wakili Mitchell Kemuma kuwa MCA maalum...

T L