• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Madai watu walilipwa kuhudhuria maadhimisho ya Jamhuri Dei Uhuru Gardens

Madai watu walilipwa kuhudhuria maadhimisho ya Jamhuri Dei Uhuru Gardens

NA SAMMY KIMATU

MAKUNDI ya vijana na akina mama waliosajiliwa kwenye miradi ya mandeleo, wanamazingira na makundi mengine ya kijamii walisafirishwa kwa matatu kutoka mitaa ya mabanda ya Mukuru kujiunga na wengine katika sherehe ya Jamhuri, Uhuru Gardens, Nairobi.

Hafla ya maadhimisho ya Jamhuri Dei 2023 inafanyika leo, Jumanne, Desemba 12.

Wakizungumza na Taifa Leo Dijitali kwa sharti la kutotambuliwa walisema kila mmoja alipewa Sh500 kuhudhuria sherehe hizo.

“Tuliambiwa na viongozi kwamba kila mmoja atapewa Sh500 endapo atajitolea kuenda Uhuru Gardens ili uwanja usionekane hauna watu wengi waliohudhuria,” mama mmoja mwanachama wa mradi wa afya ya jamii mtaani Mukuru akasema.

Makundi hayo yalikusanyika katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Hazina, South B, Kaunti Ndogo ya Starehe.

Walisafiri kwa kutumia matatu.

Katika barabara ya Lusaka, Entreprise na Lunga Lunga zilizo kitovu cha Eneo la Viwandani shughuli za uchukuzi wa magari ya usafiri wa umma zilikuwa chini.

“Sisi hutegemea wateja wetu hasa wafanyakazi katika eneo la Viwandani. Kampuni zimefungwa leo (Jumanne) kwa ajili ya Jamhuri ndiposa hatuna matatu nyingi barabarani leo,” dereva wa matatu ya Indimanje Sacco akaambia Taifa Leo Dijitali.

Katika eneo la Juakali, eneobunge la Kamukunji, mafundi wa kutengeneza masanduku ya vyuma walikuwa na kazi nyingi wakiyaunda kwa wingi, wakilenga kuuzia wazazi watoto watakapojiunga na shule za upili mapema 2024.

Machakos Country Bus, jijini Nairobi, shughuli hazikuwa nyingi kwani waliokuwa wakisafiri hawakuwa wengi.

Hata hivyo, katikati mwa jiji, wachuuzi walitawala wakiendeleza biashara zao.

Waliozungumza walisema walitumia fursa ya Sikukuu ya Jamhuri kusaka riziki kwa sababu maafisa wa serikali ya kaunti maarufu “kanjo” hawakuwa kazini.

Wachuuzi hulumbana mara kwa mara na maafisa hao wa halmashauri ya jiji.

 

  • Tags

You can share this post!

Hajuti kamwe kuuza makabeji sokoni Kongowea

Ruto: Ushuru tunaotoza wananchi umepunguzia nchi hatari ya...

T L